Idadi kubwa ya polisi nchini Senegal wamepelekwa katikati ya mji mkuu wa Dakar kuzuia mkutano mkubwa ulioitishwa na upande wa upinzani.
Kundi la vyama vya upinzani liitwalo M23, linapinga mipango ya Abdoulaye Wade ya kuwania muhula wa tatu wa urais.Watu wawili walipigwa risasi siku ya Jumatatu mjini Podor wakati wa maadamano baada ya mahakama kusema hatua ya Bw Wade ni halali.
Kundi la M23 linasema linadhamiria kuandamana hadi katika jumba la rais.
Uchaguzi katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika unatarajiwa kufanyika Februari 26.
Waandishi wa habari wanasema polisi wanawazuia waandamanaji kufika katika eneo la mkutano, liitwalo Place de l'Obelisque katikati ya jiji, ambapo viongozi wa M23 wamewataka waandamanaji wakusanyike hapo.
Mapema, mwanaharakati Alione Tune ambaye pia ni mjumbe wa M23 aliachiliwa huru na polisi bila mashataka yoyote baada ya kuzuiliwa kwa siku mbili.
Baada ya kuachiliwa huru, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa polisi walimuuliza "maswali mengi kuhusu maandamano" yaliyopangwa na M23.
Mwandishi wa BBC Abdourahmane Dia mjini Dakar amesema kuna wasiwasi maandamano ya Jumanne yanaweza yakasababisha ghasia kwa sababu hayajaruhusiwa kufanyika.
Lakini upande wa upinzani umesema una haki ya kikatiba kuandaa mikutano ya hadhara nchini kote.
Mwandishi wetu anasema miili ya waandamanaji wawili waliouawa mjini Podor siku ya Jumatatu imepelekwa Dakar kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Katiba ya Senegal inaruhusu rais kuwania mihula miwili, lakini mahakama ya kikatiba ilisema sheria hiyo haimgusi Bw wade ambaye aliingia madarakani kabla haijawekwa.
Wakati Bw Wade ameruhusiwa kuwania urais, mahakama ya katiba iliwakatalia mwimbaji Youssou N'Dour na wagombea wengine wawili wa upinzani kugombea urais.
0 Comments