Kundi la Al- Shabaab limesema linachukua hatua hiyo kwa kuwa ICRC ililisingizia kundi hilo kwa kuzuia usambazaji wa misaada, na kwamba kamati hiyo inagawa chakula kisicho bora.
Al-Shabab linathibiti sehemu za maeneo ya kaskazini na katikati mwa Somalia, ambayo kwa sasa inakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mingi.
ICRC ni mojawapo ya mashirika machache yaliyokuwa bado yanaendesha shughuli za kimisaada katika eneo hilo, na linasema halijapata taarifa za marufuku hiyo.
Shirika hilo lilikuwa limesimamisha usambazaji wa chakula mapema mwezi huu likisema wanamgambo walikuwa wamefunga njia za kusafirishia misaada, lakini bado lilikuwa linatoa msaada wa dharura na maji.
Tayari Al Shabaab lilikuwa limesimamisha kazi ya mashirika kadhaa ya misaada kwenye eneo hilo lililokumbwa na njaa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa.
Kundi hilo lililaumu mashirika hayo kwa kutilia chumvi viwango vya matatizo, kwa sababu za kisiasa, na kujaribu kuwageuza waislamu kuwa wakristo.
Katika taarifa, kundi hilo limesema "ICRC imehujumu imani ya watu wa eneo hili kwao katika majuma kadhaa yaliyiopita, na kutoa madai ya uongo kwamba mujahedeen wamezuia ugavi wa chakula".
Kundi hilo limesema asilimia 70 ya chakula ambacho wamekagua katika maghala ya ICRC sio bora kwa matumizi ya binadamu, na kwamba limeharibu tani 2000 za posho ambazo siku zake za kutumiwa zimeshapita.
Somalia inasemekana kuwa mojawapo ya maeneo hatari kabisa duniani kwa wahudumu wa mashirika ya misaada kuendesha shughuli.
Nchi hiyo haijawa na serikali kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 na imekumbwa na vita kati ya makundi mbali mbali ya wapiganaji.
0 Comments