Sifael Paul na Musa Mateja
 IMEFAHAMIKA kuwa ili kupona ugonjwa unaomsumbua mchekeshaji wa Orijino Komedi ‘OK’, Joseph Shamba ‘Vengu’ (pichani) aliyepelekwa nchini India, Alhamis iliyopita (Januari 12, mwaka huu), inagharimu dola za Kimarekani 200,000 (takribani Sh. milioni 320), Ijumaa Wikienda lina data kamili.
Vengu amekuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi yanayoshambulia seli za mfumo wa fahamu kichwani ambayo kitaalamu yanaitwa Brain au Cerebral Atrophy na kumsababishia seli za kichwani kukosa mawasiliano huku wakati mwingine akipoteza fahamu.
Kwa mujibu wa daktari mtaalamu wa magonjwa hayo, kwa dalili za Vengu, ugonjwa mwingine unaoweza kuwa jirani ni Brain Tumor ambao husababishwa na ukuaji usiokuwa wa kawaida wa seli za kichwani.
MATIBABU YAKE NI MIL. 320
Kwa mujibu wa mtandao maarufu wa kitabibu, caring.com, ili kupona kabisa maradhi kama aliyonayo Vengu, inagharimu zaidi ya milioni 320 ikiwa ni ada ya matibabu tu, achilia mbali gharama nyingine.
HATIMAYE APELEKWA INDIA
Kwa mujibu wa mmoja wa ‘memba’ wa Orijino Komedi ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji, Vengu amepelekwa katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi nchini India kwa matibabu.
JK APONGEZWA
Ndugu na marafiki wa karibu wa Vengu, wamemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kutokana na msaada wa hali na mali katika jitihada za kumpeleka Vengu kwenye matibabu nchini humo.
Vengu alianza kuugua mapema mwaka jana, hali yake ilipozidi kuwa mbaya akapelekwa Muhimbili ambapo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa zaidi ya miezi mitano.