Wafanyabiashara kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala, wamefunga maduka yao na kuyagomea mabenki kupinga kiwango kikubwa cha riba.
Benki kuu ya Uganda ilipandisha viwango hivyo mwaka jana baada ya mfumuko wa bei kufikia asilimia 20.Wafanyabiashara mjini Kampala wamesema viwango vya riba hadi asilimia 27 vinanyemelea biashara zao.
Mwandishi wa BBC alisema maduka mengi yamefungwa, na kusababisha wateja wanaosafiri kwenda Kampala kutoka nchi za Afrika Mashariki kushindwa kufanya biashara.
Umoja wa wafanyabiashara wa Kampala - ulioitisha mgomo baada ya siku mbili za majadiliano na serikali kuvunjika- umesema maduka yatafungwa kwa siku tatu.
Wamiliki wa biashara hizo pia walisema katika siku tatu zijazo wataondosha akiba zao zote kutoka mabenki ya biashara na kuacha kuhifadhi fedha kwenye hawala zao.
Mwandishi wa BBC Ignatius Bahizi alisema mamia ya watu walisimama mitaani, huku polisi wakisimamia usalama.
Kampala ni kitovu cha biashara Afrika Mashariki na wengi ambao hawakuweza kufanya biashara wametoka maeneo mengine ya Uganda, pamoja na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.
Wafanyabiashara wa mji huo wamewahi kutumia njia hiyo, Julai mwaka jana, kupinga kuporomoka kwa sarafu nchini humo na kuwepo kwa bidhaa za bei ya chini kwenye maduka ya Wachina.
0 Comments