Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), leo inatarajia kutangaza bei mpya ya umeme. Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka hiyo kukamilisha mchakato wa kupitia maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na maoni ya wadau waliopinga.

“Kesho (leo) Ewura itatangaza bei mpya za huduma za
umeme kama Tanesco ilivyowasilisha maombi mwishoni mwaka jana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Meneja Uhusiano, Titus Kaguo.Wiki iliyopita, Kaguo alisema wamekamilisha maombi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura iliyowataka kupitia upya maombi ya Tanesco kutaka kupandisha bei hiyo.
Alisema Ewura ilikwishakamilisha taratibu zote na kilichokuwa kinasubiriwa ni kutangaza bei mpya. Hata hivyo, akiwafariji wananchi akiwataka wasiwe na wasiwasi kwani wamezingatia kiwango cha mapato.

“Tuko makini kuhakikisha usawa wa huduma hii muhimu kwa jamii haiathiri pande hizi mbili ambazo kimsingi zinategemeana, nawaomba wananchi wawe wavumilivu wakati tukikamilisha kazi ya uchunguzi,” alisema.



Hatua hiyo inafanyika baada ya Tenesco kuwasilisha Ewura mapendekezo ya kupandisha gharama za umeme kwa bei ya wastani ya kuuza umeme iliyopo sasa ya Sh141 kwa uniti hadi Sh359 kwa uniti kuanzia Januari mwaka huu, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 155 ya bei ya sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando alisema sababu ya kupandisha bei ya umeme ni kiliwezesha shirika hilo kukabiliana na ongezeko la gharama za uendeshaji zinazotokana na juhudi za kuondoa mgawo wa umeme.
Mhando alisema athari ambazo zitapatikana ikiwa bei haitaongezwa ni shirika kushindwa kufanya uwekezaji na kutekeleza miradi mbalimbali ikijumuisha uuganishaji wateja wapya.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wa umeme walipinga hatua hiyo wakisema nyongeza hiyo itayumbisha uchumi wa taifa na kulitaka shirika hilo kuimarisha kwanza uzalishaji wa umeme ili liweze kupata faida.Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za mwaka mpya pia alisema Tanesco imeelemewa na mzigo.