NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kuwa balozi mzuri wa kuhamasisha wadhamini kuisaidia timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars akiwa bungeni ili iache kuwa ombaomba huku akisisitiza misingi mizuri ya uwekezaji kwa timu hiyo inahitajika.

Twiga Stars iliondoka jana usiku na ndege ya Shirika la Presion Air kuelekea nchini Namibia, lakini bado imeendelea kusota kwa kukosa fedha za kuitoa Afrika kusini hadi Namibia hivyo Shirikisho la soka nchini TFF limelazimika kukopa fedha kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inasafiri na kuendelea kusisitiza wafadhili kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali.

Akizungumza wakati akikabidhi Bendera kwa wachezaji hao, Mwalimu alisema licha ya timu hiyo kukosa fedha bado ana matumaini makubwa ya timu hiyo kurudi na ushindi kutokana na ari ya ushindi waliyokuwa nayo wachezaji na kuahidi kutumia nafasi yake Bungeni kuitetea timu hiyo ili iweze kupata misaada na udhamini.



Alisema jambo kubwa na la msingi ni TFF kushirikiana na wahisani wanapaswa kuwekeza zaidi katika soka la kina mama ambalo limeonekana kupiga hatua moja mbele zaidi ya wanaume ili kulipa sapoti kubwa na kuliendeleza.

"Sina zaidi ya kuwaahidi wachezaji hawa kuwa balozi wao mzuri nikiwa Bungeni, wadhamini ni msaada mkubwa kwao endapo watajitokeza kwani bila wao timu haiwezi kufanya lolote,hivyo TFF kwa kushirikiana nao wanatakiwa kuwekeza zaidi kwenu ili muendelee kuitangaza nchi yetu zaidi kisoka,"alisema Mwalimu.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema bado timu inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau na mpaka sasa hawajapa mdhamini mwingine zaidi ya Presicion Air hivyo imewabidi kukopa fedha ili timu iweze kuondoka Afrika Kusini kuelekea Namibia kwa ndege ya Namibia Airways.

Wachezaji walipo katika kikosi cha Twiga Stars kilichoondoka jana ni Asha Rashid, Aziza Mwadini, Ettoe Mlenzi, Fadhila Hamad, Fatuma Bushiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustapha, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Hamisi, Mwapewa Mtumwa, Pulkaria Charaji, Rukia Hamisi, Siajabu Hassan, Semeni Abeid, Sophia Mwasikili za Zena Khamisi.

Benchi la Ufundi la Twiga Stars yupo Kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa, Kocha Msaidizi Nasra Mohamed, daktari wa timu Dk. Christina Luambano na Meneja wa timu Furaha Francis.

Kiongozi wa msafara ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Lina Mhando na Naibu kiongozi wa msafara ni mjumbe wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Layla Abdallah.