Musa Mateja na Issa Mnally
MATUKIO yanayowakumba wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yanaibua vingi kuhusu nini kinaendelea ndani ya chama hicho?
Wakati Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema, akipata ajali na kupoteza maisha juzi (Jumamosi), muda mfupi kabla yake, gari la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, liliwaka moto.
Gari la Sugu aina ya Toyota Land Cruiser Amazon, liliwaka moto likiwa eneo la Kibaha Kwamatiasi, Pwani na ndani yake, mbali na Sugu, alikuwemo Mbunge wa Mbozi Mashariki (Chadema), Joseph Silinde.
Wakati Sugu na Silinde wakinusurika kifo, kwa upande wa mazingira ya ajali aliyopata Regia na kukatisha maisha yake juzi (Jumamosi ya Januari 14, 2012), yanaonesha kuwa ilikuwa ngumu kwa mbunge huyo kupona.
Regia ambaye enzi ya uhai wake, alisifika kwa ujasiri, upole na uwezo mkubwa wa kujenga hoja kwa sauti nyororo isiyo na jazba, alifikwa na mauti baada ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser VX, kupinduka mara saba.
Rogers Abdallah ambaye ni majeruhi wa ajali hiyo, aliliambia Ijumaa Wikienda akiwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kuwa Regia ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo.
“Ilikuwa saa 5:15 asubuhi. Tulikuwa tunatokea nyumbani Mbezi Makabe tunakwenda Ruvu shambani. Tulipofika Ruvu darajani, alitaka kulipita lori lakini alipoanza kulipita, tukakutana uso kwa uso na lori lingine.
“Ili kulikwepa lori, ikabidi apindishe kulia kwa kulitoa gari nje ya barabara, bahati mbaya tairi la kushoto lilipasuka, hivyo gari kupinduka mara saba,” alisema Rogers.
Marehemu Regia alikuwa mlemavu wa mguu wa kulia, ilikuwaje akaendesha gari? Rogers aliliambia Ijumaa Wikienda: “Mara kwa mara mimi ndiye huwa namuendesha lakini leo (juzi) alisema anaendesha mwenyewe na akichoka ndiyo nitamuendesha.”
Rogers aliendelea kusema kuwa ndani ya gari hilo lenye namba za usajili T 296 BSM, walikuwa ni watu nane na waliopoteza maisha ni wawili.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), John Heche, aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa mbali na Regia, mwingine aliyefikwa na mauti ni mhudumu wake anayeitwa, Teresia Simon.
Wabunge wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Mbunge wa Hai), walikuwemo Hospitali ya Tumbi ambako mwili wa Regia ulihifadhiwa kwa muda kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.
Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wabunge wa Viti Maalum, Grace Kiwelu, Raya Ibrahim na wengineo, walikuwa na nyuso za majonzi, huku baadhi yao wakishindwa kujizuia na kuangusha vilio.
Kwa upande wa wabunge wa CCM waliofika Tumbi na baadaye Muhimbili ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mbunge wa Viti Maalum Walemavu, Alshaymaa Kwegyir.
Kuhusu ajali yake, Sugu alisema kuwa alishangaa gari lake kuwaka moto kwa sababu halikuwa na hitilafu yoyote.
“Kabla ya kuanza safari ya kutokea Mbeya lilifanyiwa ‘service’, tukiwa tumeianza Pwani, tukaanza kusikia harufu ya kitu kinaungua, tukajua ni gari lingine.
“Tulipofika Kwamatiasi, kuna hiace ilitupita wakatuambia gari linawaka moto. Bahati nzuri tulikuwa na fire extinguisher, tukazima kwa sababu vyuma vya chini vilikuwa vinateketea.
“Tulikaa pale Kwamatiasi mpaka tukapewa msaada kutoka Makao Makuu ya Chadema ndiyo wakaja mafundi, wakalitengeneza na kulifikisha Dar,” alisema Sugu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa salamu za rambirambi kwa familia ya Regia na Chadema kutokana na msiba huo mkubwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema katika rambirambi hizo kuwa Regia alikuwa kiongozi shupavu wa kada zote na alishiriki kikamilifu kuwatetea walemavu ndani na nje ya bunge.
0 Comments