ZAIDI ya watu 30 wakiwepo watoto wadogo wanne wamenusurika kuzama katika Ziwa Victoria baada boti mbili kugongana eneo la Mwikoko karibu na jengo la maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 11 alfajiri, ambapo boti ya uvuvi yenye namba za usajili RMU 5234 iligongana na boti ya abiria iliyojulikana kwa jina la mv Nyanganira inayomilikiwa na Ramadhan Nyanganira.

'Chanzo cha habari' lilifika eneo la ajali na kushuhudia boti hizo zikiwa zimeharibika huku kukiwa na madai ya watu kutoonekana baada ya baadhi yao kuokolewa. Baadhi ya mashuhuda na abiria walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa boti hizo na kutozingatia sheria za unahodha.

“Kabla ya ajali kutokea kama meta mia moja hivi, abiria walimuambia nahodha aangalie mbele boti iliyokuwa ikija, lakini alishindwa kumiliki vyema boti hiyo na alipokata kona tu boti ya uvuvi iligonga katikati,” alisema mmiliki wa boti hiyo, Nyanganira na kuongeza:


"Hatuwezi kusema kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha, ukweli utapatikana baada ya siku moja au mbili”. Abiria wa boti hilo aliyejitambulisha kwa jina la Eunice Maagi, mkazi wa Kiabakari aliyedai alikuwa akitoka kwenye msiba katika kijiji cha Kibuyi wilayani Rorya, alisema kuwa hadi alipookolewa na kupata fahamu vizuri, hakuna mtu yeyote aliyelalamika kama ndugu, jamaa au rafiki yake haonekani.

“Hakuna niliyemsikia analalamika kuwa amepotelewa na mtu sijui kwa kuwa bado
tumechanganyikiwa na pia kutojuana kutokana na kila mtu kuwa na safari yake, lakini sisi tulikuwa kama sita na wote tumeokolewa na tupo salama,” alisema Maagi.