POLISI Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya mkoani Mara inawashikilia watu watatu kwa
tuhuma za kupatikana na magunia matano ya bangi.

Watu hao walikamatwa kwenye msako unaoendelea dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya kwa lengo la kudhibiti uhalifu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Justus Kamugisha amesema ofisini kwake kuwa watu hao walikamatwa katika kijiji cha Kiterere Kata ya Bumera katika Tarafa ya Nchage wilayani Tarime.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Sabah Chacha (22) mkazi wa kijiji cha Kwembe, Samweli Mwita [43] na Dickson Sabah [31] wakazi wa kijiji cha Bisarwi Wilaya ya Tarime.

Magunia hayo matano yalikuwa na bangi kavu yenye uzito wa kilo 150 na ilikuwa ikisafirishwa kwenda Kenya kupitia njia za panya. Alisema baada ya upelelezi wa Polisi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Wakati huo huo mtembea kwa miguu Fred Joseph (9) mwanafunzi wa Darasa la Tatu katika Shule ya Msingi ya Turwa amegongwa na gari na kufa papo hapo.

Mtoto huyo aligongwa na gari lenye namba za usajili T. 579 BCS likiendeshwa na Joseph Chacha (23) mkazi wa Magena karibu na Hoteli ya CMG Barabara ya Tarime- Musoma.

Gari hilo linadaiwa kutokea Tarime kwenda Buhemba.

Kamanda Kamugisha alisema dereva anashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi na ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.