Ofisa wa Habari Tanesco,Badra Masoud.

Ibrahim Yamola
SHIRIKA la Umeme Nchini (Tanesco), linakabiliwa na uhaba mkubwa wa mita za Luku, kiasi cha kufanya baadhi ya wateja waliolipa zaidi ya miezi minne iliyopita kushindwa kupata huduma hiyo.

Pamoja na wateja kuahidiwa kuanza kupata huduma ya Luku mwishoni mwa mwaka, hakuna mteja aliyepata mita hizo licha ya kulipia toka mwaka jana.

Wateja hao waliulalamikia uongozi wa Tanesco kwa kuchelewesha kutoa huduma huku ikiacha jambo hilo kuwa kimya bila taarifa kwa wateja.

“Mimi nimeambiwa kuwa kuna uhaba wa mita lakini nimelipa tokea mwezi Oktoba mwaka jana, wangekuwa wanatoa taarifa kwa wateja, pesa hizo zingeweza kupata matumizi mengine hadi watakapokuwa tayari,” alieleza mama mmoja mkazi wa Tabata aliyejitambulisha kama mama Yvonne.

Richard Kasele, mteja wa Tanesco mkazi wa jijini Dar salaam, alisema inasikitisha kwa shirika hilo kushindwa kutoa taarifa kama hizo kwa wateja na hivyo kusababisha watu kuhangaika kufuatilia mara kwa mara katika ofisi zao bila kupewa majibu ya uhakika.



Baadhi ya wateja ambao walilipia waliishia kupatiwa njia za umeme bila ya kuwekewa mita kwa miezi kadhaa na wengine walilazimika kuunganisha nishati hiyo muhimu ili kupata huduma.

“Tumewapatia pesa lakini huduma wanaleta nyaya hadi nyumbani, ila mita hawaweki, ukiunganisha umeme wanakukamata na kukutoza faini, hii sio haki kwani mita ni mali yao na wenyewe wanahitaji kuweka ili tunapolipa wapate mapato na kuboresha huduma,” alieleza Richard Mbasha ambaye alikuwa akifuatilia umeme katika ofisi za Tanesco Tabata katika kituo cha reli ya Tazara.

Ofisa Habari wa Tanesco Badra Masoud, alikiri kutokuwepo kwa huduma hiyo toka mwaka jana huku akisema tatizo hilo litamalizika mwishoni mwa wiki hii.

“Tatizo hili lilikuwepo na lilisababishwa na msambazaji wetu aliyetarajia kutuletea kuchelewa lakini kitu kizuri ni kwamba kuanzia Ijumaa hii (kesho kutwa) zitaanza kupatikana na wateja wote wataanza kupatiwa huduma hiyo,” alisema Mosoud.

Akifafanua kuhusu tatizo la umeme kukatika mara kwa mara, Masoud alisema ni tatizo la kawaida na halihusiani na mgao wa umeme.

“Kwa sasa hatuna mgao wa umeme na kinachotokea kwa tatizo la kukatika kwa umeme ni kutokana na tatizo ambalo ni la kiufundi na ndio maana huduma hurejea kwa muda mfupi,” alisema Masoud.

Aidha, Masoud aliwatahadharisha wananchi kutokubali kufanyiwa huduma ya kupata umeme ama tatizo lolote la kiufundi na mafundi wasio na vitambulisho.

“Wananchi wanatakiwa kutambua kuna baadhi wa watu wanajiita wafanyakazi wa Tanesco kumbe ni matapeli (vishoka) wenye lengo la kuwaunganishia njia za umeme na huduma zingine kutowakubalia kama hawana vielelezo vinavyoonesha wametoka Tanesco,” alisema Masoud
.