Strauss-Kahn anahojiwa na polisi kwa tuhuma za biashara ya ngono.

Aliyekuwa mkuu wa Shirika la Fedha Duniani Bwana Strauss-Kahn, anahojiwa na polisi nchini Ufaransa kama mshukiwa wa sakata ya biashara ya ngono.
Bwana Strauss-Kahn ambaye pia aliwahi kuwa mstari wa mbele katika kuwania urais nchini humo, amezuiliwa katika kituo cha polisi mjini Lille kaskazini mwa Ufaransa.
Polisi wamehoji makahaba kadhaa waliodai kuwahi kuwa na uhusiano wa kingono na bwana Strauss-Kahn.
Hata hivyo amesisitiza kuwa hakufahamu ikiwa wanawake hao walikuwa makahaba.
Bwana Strauss-Kahn alijiuzulu wadhifa wake kama mkuu wa Shirika la Fedha duniani mwezi Mei mwaka 2011 baada ya kukabiliwa na tuhuma za jaribio la kumbaka mfanyakazi wa hoteli mjini New York Marekani.
Hata hivyo baadaye kesi hiyo ilitupiliwa mbali.
Katika uchunguzi huu polisi nchini Ufaransa tayari wanawachunguza wanaume wawili kwa makosa ya kuunda mitandao ya ukahaba na kufuja pesa za shirika la IMF kwa kulipia biashara za ngono.