Diwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Maboga Wilaya ya Iringa Vijijini, Fulgence Lutego (41), ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi na kisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi, Wilaya ya Iringa, akituhumiwa kuhusika katika mauaji ya mwendesha pikipiki, Denis Kiluka, aliyeuawa na kutupwa korongoni.

Diwani Lutego, anadaiwa kufanya mauaji hayo akishirikiana na Benson Mdongwe (30) na Joel Boniface (39), wakazi wa Kijiji cha Makombwe, Kata ya Maboga Tarafa ya Kiponzelo wilayani hapa.
Marehemu Kiluka anadaiwa kuuawa muda mfupi baada ya kufika kijijini Makombwe na kukutana na Mdongwe na baadaye Diwani Lutego.
Watuhumiwa hao walisomewa kosa hilo jana kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Mary Senapee, huku wakitakiwa kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Lilian Ngilangwa, kuwa watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa na Jamhuri kwa kosa la mauaji ambalo ni kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Senapee alisema kuwa watuhumiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na kuamuru warejeshwe rumande kwa vile kesi hiyo haina dhamana.
Kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2012, iliahirishwa hadi kwa ajili ya kutajwa Machi 13, mwaka huu.