Askari polisi akionyesha karatasi iliyoandikwa maandishi ya kiarabu kwa waandishi wakati wa mkutano na mjini Songea jana, karatasi hiyo pamoja na hirizi zilikutwa kwenye mifuko ya watuhumiwa wa mauaji yanayohusishwa na ushirikina mjini humo. Picha na Joyce Joliga


WENGINE WAWILI WAUAWA, WANAHARAKATI WATAKA RC, DC, IGP WAFUKUZWE KAZI
Waandishi Wetu
HALI katika Mji wa Songea, Ruvuma bado ni tete. Baada ya watu wanne kuuawa na polisi Jumatano iliyopita, watu wengine wawili wameuawa kwa kupigwa na wananchi juzi.Watu hao ambao ni wanaume, walishambuliwa kwa marungu, mawe na mapanga na kufariki dunia baadaye wakiwa kwenye matibabu. Wananchi waliwashambulia baada ya kuwatuhumu kuhusika na vitendo vya mauaji mkoani humo.

Juzi, Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma liliwakamata na kuwaweka mahabusu askari wake wanne wanaotuhumiwa kutumia risasi za moto na kusababisha vifo vya watu wanne Jumatano wiki hii, wakati wananchi waliokuwa wakipinga mauaji dhidi ya wenzao tisa kwa imani za kishirikina walipopambana na polisi. Watu 41 kujeruhiwa.

Fujo za juzi zilitokea katika Mtaa wa Mkuzo, Songea mara baada ya wananchi kuwakamata watu hao wawili ambao walishindwa kujieleza wakati wakihojiwa. Mbao ya hao, pia alikuwepo mwanamke mmoja ambaye alifanikiwa kutoroka.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, watu hao walijitetea kuwa wao ni mafundi ujenzi na walikuwa wakimtafuta mtu ambaye hata hivyo, walishindwa kumtaja jina ili awauzie kiwanja. Baada ya kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha, wananchi waliwataka waeleze walipotoka na wameshaua watu wangapi.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mkuzo,
John Moyo alisema wananchi hao walifanya fujo hizo kwenye ofisi yake baada ya kuwafikisha.

Moyo alisema wananchi walipowahoji na kuona wakishindwa kujieleza walianza kuwashambulia kwa kuwapiga na kuwajeruhi vibaya.



Baada ya kushindwa kuwadhibiti, alisema alipiga simu polisi ambao walipowasili eneo la tukio walilazimika kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu ya kutoa machozi na kuwapeleka watu hao hospitali.

Wakiwa hospitalini, watu hao walifanyiwa upekuzi na kukutwa wakiwa na hirizi moja kubwa rangi nyeusi pamoja na karatasi nyeupe iliyoandikwa kwa lugha ambayo haikuwa rahisi kusomeka.

Walipoulizwa majina yao, mmoja alisema anaitwa Juma na mwenzake ni Gervase. Katika hali iliyoashiria kuwa Gervase hakutaka atajwe, alimuashiria mwenzake kwa kumbana na pingu.

Wakati huo Gervase alikuwa amevimba uso na alionekana kuishiwa nguvu na hali yake kuzidi kuwa mbaya.

RPC, hosipitali
Baadaye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema Gervase alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu mapokezi na mwenzake Juma pia aliaga dunia saa chache baadaye.

“Haikuwa rahisi kwa watu hao kupona kwani hali zao zilikuwa mbaya sana. Walikuwa wamejeruhiwa vibaya maeneo ya kichwani na vifo vyao vimetokana na kupoteza damu nyingi,” alisema Dk Ngaiza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,
Michael Kamhanda amethibitisha kutokea kwa tukio akiwasihi wananchi waache kuchukua sheria mkononi na badala yake watii sheria bila kushurutishwa pindi wanapomuhisi mtu kuwa ni mhalifu.

“Kwa kweli nasikitishwa na kuumizwa sana na matukio yanayoendelea. Naomba wananchi watulie waache kuuana kwani vitendo hivyo ni vya kinyama na ni uvunjifu wa amani. Tunawaomba wasaidiane na polisi ili tuweze kudhibiti au kutokomeza kabisa wimbi hili la mauaji katika mji wetu,” alisema Kamhanda.

Vikao

Kutokana na wasiwasi uliotanda katika Mji wa Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu kwa upande mmoja na Kamanda Kamhanda kwa upande mwingine jana kutwa waliripotiwa kushinda katika vikao tofauti vyenye lengo la kurejesha utulivu.

Mwambungu alikuwa na kikao na waendesha pikipiki maarufu kwa jina la Yeboyebo jana mchana katika Ukumbi wa Klabu ya Songea ambacho kilikuwa kikihamasisha ulinzi shirikishi ili kukomesha mauaji hayo.

“Madreva pikipiki mna mchango mkubwa sana maana abiria wenu walio wengi mnawafahamu vilivyo hivyo ni vyema kama kuna mtu mna wasiwasi naye mkatoa taarifa polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa,” alisema Mwambungu.

Kamhanda kwa upande wake alikuwa na vikao tofauti katika kambi za polisi na mara ya mwisho ilielezwa kwamba alikuwa Ofisi za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Songea.

Katika hatua nyingine, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine Songea, wamelalamikia milipuko ya mabomu ya juzi jioni kwamba iliwaathiri kwenye mitihani.

Mmoja wa wanafunzi hao, Hofe Seregius alisema milipuko ya mabomu ambayo yalitua jirani na chuo chao na kwamba yaliwafadhaisha kiasi cha kushindwa kuendelea na mitihani ya historia, hivyo wanataka uongozi wa chuo kuwaruhusu kurudia mtihani huo.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Donatus Komba alikiri kuwapo kwa taharuki kwa wanafunzi akisema Polisi walitumia nguvu kubwa dhidi ya wananchi.

Wanaharakati waja juu

Mtandao wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHARiNGON) umelaani kitendo cha polisi kuua raia kwa risasi katika maandamano hayo na kumtaka Rais kuwawajibisha Mkuu wa Mkoa Ruvuma na Kamanda wa Polisi wa Mkoa kwa kuwa chanzo cha vurugu hizo.

Watendaji wengine waliopendekezwa kuwajibishwa ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Thomas Ole Sabaya na watendaji wakuu wa Manispaa ya Songea.

Akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana, Mratibu wa SAHRiNGON Tawi la Tanzania, Martina Kabisama alisema wahusika hao wameshindwa kutimiza wajibu wao jambo lililosababisha wananchi kuandamana kwa amani na kushambuliwa na polisi.

Alisema taarifa za matukio ya watu kuuawa kwa kile kilichoelezwa ni imani za kishirikina zilianza kujitokeza Novemba mwaka jana na taarifa zilifika polisi na hadi wananchi wanafikia hatua ya kuandamana, wahusika hawakuonekana kuchukua hatua.

“Ni jambo la kushangaza kwa polisi hao kwenda kuvamia maandamano ya amani na kuua raia. Kitendo hicho tunakilaani sababu wananchi waliandamana kwa amani ikiwa ni namna yao ya kupaza sauti baada ya polisi kushindwa kuchukua hatua dhidi ya matukio hayo,” alisema.

Alisema kitendo hicho cha polisi ni kinyume na haki ya kuishi kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 13 ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Alisema kitendo hicho pia kimekiuka haki ya mkusanyiko kama inavyoelezwa katika Ibara ya 21 kifungu cha kwanza, haki ya kusikilizwa na kutoa maoni Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema tukio la maandamano na vurugu zilizotokea ni matokeo ya Serikali kushindwa kuchukua hatua kwa wakati tangu mauaji ya raia yaliyohusishwa na imani za kishirikina yalipoanza kutokea Novemba mwaka jana.

Kabisama alishauri viongozi na watendaji serikalini kujenga utamaduni wa kuchukua hatua dhidi ya matukio mbalimbali yanapotokea kabla ya kusababisha athari.

“Kumejengeka tabia ya Serikali kuchukua hatua baada ya migomo na maandamano kutokea. Tumeshuhudia mgomo wa madaktari watu wamekufa ndipo Serikali inachukua hatua na hili la Songea watu wameandamana na kupoteza maisha ndipo Serikali inachukua hatua. Kitendo hiki cha kushindwa kuchukua hatua kwa wakati ndicho kinacho sababisha wananchi kuchukua sheria mkononi,” alisema.

CCK chapanga kushtaki polisi
Chama cha Kijamii (CCK) kimesema kinatarajia kulishtaki Jeshi la Polisi mara baada ya kukamilika kwa mpango wa ukusanyaji wa taarifa kuhusu mauaji yaliyofanywa na Polisi huko Songea.

Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda alisema jana katika taarifa yake: “Hatua ya kulipandisha jeshi la Polisi kizimbani itakuwa ni tukio la kihistoria katika kuitikia wito wa kutetea haki za wananchi wetu.” Hata hivyo, hakusema ni lini hatua hiyo itachukuliwa.

Alisema chama hicho kimependekeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iingilie kati sakata hilo ili kujua ni kwa namna gani wahusika mbalimbali walivyochangia mauaji hayo.

“Pia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu achunguzwe kuhusu kauli yake kwamba polisi waliwaua wananchi waliokuwa wakiandamana kuelekea kwenye majengo ya Serikali,” alisema Akitanda.

Akitanda alisema chama hicho pia kinapendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kuhojiwa kuhusu matukio ya mauaji ya polisi ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara hapa nchini.

Habari hii imeandikwa na Kwirinus Mapunda na Joyce Joliga, Songea; Raymond Kaminyoge, Geofrey Nyang'oro na Taus Ally, Dar.