Elvan Stambuli na Makongoro Oging'

 SIRI ya ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe ambaye amesema kuwa ana matatizo kwenye Uboho (Bone marrow), imefichuka.
Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela hadi sasa bado wataalamu katika Hospitali ya Apollo nchini India anakotibiwa wanafanyia uchunguzi uboho wake, lakini daktari mmoja amefichua siri ya ugonjwa wa sehemu hiyo.
TATIZO LA KITAALAMU
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema binadamu akiwa na matatizo katika uboho yaani urojo ulio katikati ya mfupa ni tatizo zito.
“Kwa kuwa Dk. Mwakyembe hajafafanua katika bone marrow (uboho) yake kumekutwa na nini kama walivyomuambia madaktari wa Apollo India lakini nakuhakikishia kuwa mtu yeyote aliye na matatizo sehemu hiyo ya mwili huwa ana tatizo zito siyo jepesi.
“Kwa mfano, katika urojo huo mtu anaweza kugundulika kuwa na Leukemia (kansa ya damu), ambapo bone marrow huzalisha white cells (seli nyeupe) ambazo siyo za kawaida, hivyo mgonjwa kujikuta akiwa na aplastic anemia yaani uboho hushindwa kuzalisha red blood cells (seli nyekundu za damu) na kupata kansa ya damu, ugonjwa uliomuua Nyerere, (Julius Kambarage ),” alisema daktari huyo.
Daktari huyo alifichua siri zaidi kwa kuongeza kusema kwamba binadamu akiwa na tatizo katiba uboho anaweza pia kujikuta akipatwa na ugonjwa unaoitwa kitaalamu lymphoma ambao hudhuru uzalishaji wa chembechembe za damu ( blood cells) mwilini.

TIBA YAKE
Alipoulizwa mtu akiwa na hali hiyo anaweza kupewa tiba gani, daktari huyo alisema matibabu yanategemea na jinsi ugonjwa ulivyoathiri uboho.
“Tiba yake inaweza kufanywa kwa kutumia dawa mbalimbali au kwa kubadilishwa damu au ikibidi kutia kwenye mifupa uboho mwingine, ” alifafanua daktari huyo.
Hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya Dk. Mwakyembe ambaye anatetewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Samweli Sitta anayedai kuwa mbunge huyo wa Kyela amelishwa sumu lakini Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba hivi karibuni alisema kuwa naibu waziri huyo hajalishwa sumu.

RIPOTI YA HOSPITALI YA INDIA
Naye Dk. Mwakyembe akadai kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo ya India anakotibiwa.
“Ripoti inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua…Lakini vyombo vyetu vya dola vinapelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu kwamba ‘sikulishwa sumu’, ‘sikulishwa sumu,” alisema Mwakyembe katika taarifa hiyo.Aliongeza: “Nimelazimika kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari uliofanyika kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa, sikunyweshwa sumu.”