MAHAKAMA inaangalia njia mbadala ya kuepuka adhabu ya kifungo katika makosa ya jinai na hasa yenye adhabu ndogo.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Sheria inayoadhimishwa jana Dar es Salaam katika viwanja vya Mahakama Kuu.
Alisema mwaka huu, kaulimbiu ya Siku ya Sheria ni ‘Adhabu Mbadala Katika Kesi za Jinai’.
“Kitakachojadiliwa kesho (jana) ni namna ya kuangalia adhabu mbadala katika kesi hizi za jinai na hasa zenye adhabu ndogo, si kila kosa adhabu iwe kifungo, tunaweza kupata adhabu zingine,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema kuna idadi kubwa za kesi za jinai katika Mahakama za ngazi zote kuliko kesi nyingine na pia kuna msongamano magerezani ambavyo vitazungumzwa katika maadhimisho hayo.
Jaji Othman alisema maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka wakati wa mwanzo wa shughuli za mwaka za Mahakama, yalianza kuadhimishwa mwaka 1999 na yote yaliadhimishwa Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama na pia kupata washiriki wengi.
Akizungumzia adhabu ya kunyongwa, Jaji Mkuu alisema adhabu hiyo imepingwa mahakamani na kuna watu wamefungua kesi kupinga sheria inayotoa adhabu hiyo kwa sababu ni kinyume cha sheria. Alisema pia utafiti unafanywa na Tume ya Haki za Binadamu kuangalia adhabu hiyo.
Jaji Mkuu alisema Mahakama imeandaa utaratibu wa kuendesha mafunzo kwa mahakimu na majaji wanaokuwa kazini ili kuwajengea zaidi uwezo. Akizungumzia mafunzo hayo, Jaji Mkuu alisema kwa muda mrefu hawakuwa na utaratibu huo na badala yake jaji au hakimu akitoka chuoni, alikabidhiwa kituo cha kazi bila mafunzo zaidi ya kazi.
“Kwa miaka mingi hatukuwa na utaratibu wa kuwapa mafunzo ya uzoefu mahakimu na majaji, kwa kuwa Chuo cha Mahakimu cha Lushoto kinafundisha nadharia tu, wakihitimu pale basi, wanakabithiwa majalada wanaanza kusikiliza kesi,” alisema Jaji Othman.
Pia aliitaka Serikali kuweka katika sera zake utaratibu wa kuijengea jamii welewa wa sheria mbalimbali ili kuiwezesha kuepuka makosa mengine, kwa kuwa kuna watu wanatenda makosa kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria.
0 Comments