Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Februari 5, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Mji wa Wurzburg wa Ujerumani, Mheshimiwa George Rosenthal.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanza, Meya Rosenthal ameambatana na madiwani wanne, mkewe, Hanna Rosenthal na binti yake, Lisa Rosenthal.
Ujumbe huo wa mji wa Wurzburg unatembelea Jiji la Mwanza kwa muda wa wiki moja ikiwa ni ziara ya kirafiki kati ya miji hiyo miwili uhusiano wa kindugu.
Mji wa Wurzburg ulianzishwa miaka 1,300 iliyopita, una vyuo vikuu vitatu na wanafunzi kiasi cha 30,000 wanaosoma katika vyuo hivyo.
Mji wa Wurzburg unalisaidia Jiji la Mwanza katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na utunzaji mazingira, afya, nishati. Pia miji hiyo miwili ina program ya kubadilishana wanafunzi kwa maana ya wanafunzi wa miji hiyo miwili kutembeleana na pia Jiji la Wurzburg linaisaidia taasisi za kijamii za Jiji la Mwanza.
Rais Kikwete amemwambia Meya Rosenthal kuwa Tanzania na Ujerumani zina uhusiano mzuri na wa karibu na Serikali yake imedhamiria kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano huo.
Rais pia amesifu uhusiano huo wa kindugu kati ya miji ya Mwanza na Wurzburg na ametaka miji hiyo kuimarisha uhusiano huo kwa sababu ni muhimu na unanufaisha pande zote mbili. Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Mwanza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
05 Februari, 2012
Rais pia amesifu uhusiano huo wa kindugu kati ya miji ya Mwanza na Wurzburg na ametaka miji hiyo kuimarisha uhusiano huo kwa sababu ni muhimu na unanufaisha pande zote mbili. Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Mwanza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
05 Februari, 2012
0 Comments