Na Lydia Churi, MAELEZO, Dodoma
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inakubali kuwa wastaafu kupewa mkataba wa kuendelea kufanya kazi si sahihi na kuahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi.
Akifanya majumuisho wakati wa mjadala wa Azimio la kuridhia mkataba wa vijana wa Afrika (The African Youth Charter) waziri Nchimbi alisema hatua ya wastaafu kupewa mikataba ya kuendelea na kazi inawanyima vijana haki ya kupata ajira katika taasisi mbalimbali.
Akizungumzia suala la maadili kwa vijana Mheshimiwa Nchimbi alisema hivi sasa vijana wakiwemo baadhi ya viongozi wanaotoa michango yao juu ya mambo mbalimbali katika mitandao kama vile facebook na twitter wanatumia lugha zisizojenga na badala yake aliwataka kutoa michango isiyokuwa na madhara kwa vijana wa taifa hili hasa ile inayotumia lugha zinazojenga ili kulinda maadili ya Mtanzania.
Aliwataka viongozi kuwa wa kwanza kupiga vita matumizi mabaya ya mitandao na kuacha tabia za kulipiza visasi pale wanapokosana na wenzao kwani hizo si sifa za kiongozi bora. “kiongozi bora na imara ni yule mwenye tabia ya kusamehe, alisema”.
Kuhusu mchakato wa kutafuta vazi la taifa waziri huyo alisema wizara yake inatekeleza maagizo yaliyotolewa na bunge na kuwaomba wabunge kuwa wa kwanza kuunga mkono wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inapotekeleza maagizo hayo. Aliongeza kuwa kamati iliyoteuliwa kutafuta vazi la taifa ni makini kwa kuwa imeundwa na watu makini waliotoka kwenye kada mbalimbali.
Awali akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) Peter Serukamba alisema suala la wastaafu kupewa mkataba wa kuendelea na kazi halifai kwa kuwa linawanyima vijana haki yao ya kupata ajira. Alitoa mfano kuwa hivi sasa wenyeviti wa bodi wengi ni wastaafu ambapo ilipaswa nafasi hizo kuchukuliwa na vijana.
Alisema suala la uzoefu kuwa miongoni mwa sifa za kupata ajira si haki kwa kuwa linawanyima vijana nafasi ya kupata ajira hizo. Alisema vijana wawapo vyuoni hupatiwa muda wa kufanya mazoezi ya kazi na hivyo kuwa na uzoefu wa kutosha.
Bunge limeridhia mkataba wa kimataifa wa vijana isipokuwa limeridhia kwa stara ibara mbili zinazohusu sera ya taifa ya vijana na suala la vijana wa kike wanaopata ujauzito au kuolewa kabla ya kumaliza elimu zao kupewa fursa ya kuendelea na masomo.
Bunge limeridhia kwa stara ibara hizo kwa kuwa Sera ya Taifa ya Vijana kwa taratibu za nchi yetu hupitishwa na baraza la mawaziri na sheria hutungwa na bunge wakati mkataba unasema Sera itapitishwa na kukubaliwa na bunge na kufanywa sheria.
Kwa upande wa elimu kwa vijana wa kike waliopata ujauzito masomoni, mkataba unataka wasichana wa kike wanaopata ujauzito masomoni kuepwa firsa ya kuendelea na masomo wakati sheria za nchi yetu bado haziruhusu vijana wa kike waliopata ujauzito masomoni kuendelea na masomo.
0 Comments