Serikali ya Uganda imetia saini makubaliano ya uzalishaji mafuta na kampuni ya Uingereza ya jijini London, Tullow oil.
Mkataba huo unafungua njia kwa uwekezaji wa dola bilioni 10 katika kiwanda cha kusafisha mafuta na bomba la kusafirisha mafuta yasiyosafishwa.
Tullow oil itauza robo tatu ya eneo lake la ziwa Albert kwa kampuni ya Uchina CNOOC na kampuni ya Ufaransa ya Total.
Mkataba huo una thamani ya dola bilioni 2.9 na unamaliza mvutano na serikali ya Uganda kuhusu kodi katika siku zijazo.
Waziri wa mafuta wa Uganda Irene Muloni amesema Tullow imekubali mabadiliko ya vipengele vya serikali vya "kuimarisha" ambavyo vitajumuishwa katika mkataba wa kutetea kampuni dhidi ya hasara iwapo serikali itabadili sheria za kodi.

Msemaji wa Tullow George Cazenove amesema kampuni imeridhika na vifungu hivyo.
"Ni muhimu kukumbuka kuwa maendeleo ya bonde la Ziwa Albert yatakuwa ya muda mrefu kwa maendeleo ya Uganda kwa miaka mingi - kuna mafuta mengi sana pale," Bw Cazanove ameiambia BBC.
"Kutakuwa na kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda na bomba pia."
Hazina ya mafuta na kiwanda cha kusafisha vitakuwa vinatosha kukidhi mahitaji ya Uganda, na pia baadhi ya nchi majirani ikiwemo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.