Na Khadija Mngwai
UONGOZI wa Yanga umesema mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek itachezwa usiku.
Yanga itamenyana na Wamisri hao Machi 2 au 3, mwaka huu jijini Cairo, lakini taarifa kutoka Misri walizopewa viongozi wa timu hiyo, zinasema mechi hiyo itachezwa usiku.
Akizungumza na Chanzo hiki, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema wamepata taarifa za chinichini kuwa mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa mbili, hivyo watalazimika kufanya mazoezi katika muda huo pindi watakapotua nchini humo.
“Kutokana na taarifa hizo, tumeona bora tuondoke siku ya Ijumaa na Jumamosi tucheze kutokana na mazingira ya hali ya hewa ya baridi ili isiwachoshe wachezaji.
“Licha ya kutambua mchezo huo unachezwa usiku, lakini tukiwa kama viongozi hatujapata taarifa yoyote, kila kitu tunasikia juujuu tu. Tumezungumza na TFF wamesema bado wanaendelea na mawasiliano, sijajua wenzetu wana maana gani.
“Sasa tunafuatilia suala la usafiri hatujajua ni ndege gani hadi sasa. Bado hatujui tutafikia katika hoteli gani au tunaweza kulala Airport, kwa ujumla bado hatujawa na uhakika. Vilevile hatutambui aina ya uwanja tunaokwenda kuchezea iwapo ni wa nyasi bandia au kawaida.”
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Februari 18, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilifungana bao 1-1.
0 Comments