Waandishi Wetu
KADRI uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki unavyokaribia, ndivyo vyama vyenye upinzani mkuu, CCM na Chadema vinavyozidi kukabana. Jana kwa vyakati tofauti, vyama hivyo viliendelea na kampeni zake maeneo mbalimbali ya jimbo hilo vikikusanya mamia ya wafuasi na wapenzi wake.
Wakati kampeni za Chadema zikiwa zinaongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kwa upande wa CCM, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ndiye aliyeonekana kung'ara jana.
Lakini tofauti na Mbowe, ambaye alikuwa akinadi sera muda mwingi, Lusinde alionekana kukishambulia Chadema kwa tuhuma mbalimbali.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyija jana kwenye Uwanja wa Ndarasero, Usa River, Mgombea wa CCM, Sioi Sumari alisema atatumia Ilani ya chama chake kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Pia aliahidi kutimiza ahadi zilizoachwa na mbunge marehemu Baba yake, Jeremia Sumari huku akisema atatilia mkazo tatizo la ajira kwa vijana na kutatua shida za maji na ardhi ili kuwaletea maendeleo wananchiu wa Arumeru.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Meneja wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba, Wabunge, Stephen Ngonyani (Korogwe Vijijini), Said Nkumba (Sikonge) na Zainab Kawawa (Viti Maalumu).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mikutano ya kumnadi mgombea wake Joshua Nassari juzi na jana, alitoa mwaliko kwa wanachama na wafuasi wote wa chama hicho kwamba wafike kwenye mkesha wa kusubiri matokeo ya uchaguzi huo eneo la Leganga, jirani na Halmashauri ya Meru.
Mbowe alisema mara baada ya kubandikwa kwa matokeo katika vituo vyao, wapigakura kwa pamoja wanapaswa kuelekea katika eneo la Leganga kusubiri matokeo ya uchaguzi.
Msimamizi wa Uchaguzi huo, Trasias Kagenzi mara kadhaa amekuwa akiwasihi viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kutokuwa na wasiwasi kwa maelezo kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Mkuu wa Oparesheni ya Polisi katika uchaguzi huo, Naibu Kamishna, Isaya Mngulu alisema polisi ndiyo wenye jukumu la kusimamia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi huo na kwamba wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu mchakato wa upigaji kura.
Mbowe mita 103
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mulala, Kata ya Songoro nyumbani kwa mgombea wa chama hicho, Nassari, Mbowe alisema: “Naomba mara baada ya kupiga kura, utakaa mita 103 kutoka kwenye kituo, hadi matokeo ya kituo chako yatakapobandikwa, chukua kanga, baiskeli, punda, gari au usafiri wowote tukutane Usa River ambapo tutafanya mkesha wa kusubiri matokeo.”
Alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba kuna shinikizo la kumtaka Msimamizi ya Uchaguzi, Kagenzi atangaze matokeo tofauti ikiwa Chadema watakuwa wameshindwa.
“Ndugu zangu msigope kitu, tutakwenda kulala wote Usa River kusubiri matokeo yetu na kama wakitubia haki ya Mungu safari hii hatutakubali,” alisema Mbowe.Mbowe aliwataka polisi siku ya uchaguzi kuwaacha Chadema na CCM wachuane wenyewe kwani kazi yao ni kulinda amani na siyo kuilinda CCM.
Mapema Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliwataka wakazi wa jimbo hilo, wasiwe na hofu ya wingi wa polisi katika maeneo yao akisema haijawahi kutokea hata siku moja bunduki ikazidi nguvu ya umma.
“Makamanda jitokezi kupiga kura kuanzia saa 12:00 jioni mkimaliza msubiri matokeo na baada ya hapo tukutane Usa River na hapo kutakuwa na makada wenzenu kusubiri matokeo.”
Kwa upande wake, Nassari aliwataka wakazi wa kata hiyo kujitokeza kumpigia kura Jumapili ili awe mbunge wao kwani wanamfahamu vizuri kuwa ni mgombea pekee ambaye anaweza kuwasaidia katika jimbo hilo.
“Leo nipo hapa nyumbani nimesoma hapa na huu uwanja tulikuwa tukicheza mpira, hapa kuna diwani wa CCM kama mnakumbuka shule ilifungwa kwa kukosa vyoo. Miaka 50 ya Uhuru leo wanakuja tena kuomba waendelee kuongoza sasa wanaweza nini kama hata choo kinawashinda?” alisema Nassari.
Nassari alisema kama akichaguliwa atahakikisha anakabiliana na matatizo katika sekta ya elimu kwani halmashauri hiyo imetenga zaidi ya Sh3.9 bilioni za maendeleo mwaka huu lakini hadi sasa hazijulikani zimefanya nini.
Katika mkutano huo, Viongozi wawili wa CCM, akiwemo Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Tawi la Mulala, Eribariki Manjeka alirudisha kadi yaCCM na kujiunga na Chadema pamoja na William Nassari ambaye aliwahi kuwa Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM katika kata hiyo.
Imeandaliwa na Neville Meena, Edwin Mjwahuzi, Mussa Juma na Peter Saramba.
0 Comments