Raia wa Uingereza aliyetekwa nyara nchini Kenya na mumewe kuawa ameachiwa huru baada ya kuzuiliwa miezi sita nchini Somalia.
Judith Tebbutt amewasili mjini Nairobi baada ya kulipiwa kikombozi na jamaa zake.
Mama huyo wa miaka 56 alikuwa amezuiliwa eneo la Adado, huko Somalia.
Mumewe David Tebbutt alipigwa risasi na genge la watu sita walioshambulia hoteli walimokuwa kwa likizo iliyoko eneo la Kiwayu kisiwani Lamu.Yeye anashughulika na huduma ya jamii na huwa kiziwi.
Bi Tebbutt anahudumiwa na maafisa katika ubalozi wa Uingereza mjini Nairobi kabla ya kurejeshwa nyumbani ambapo ataungana na jamaa zake.
Judith Tebbutt alitekwa nyara Septemba 11 mwaka jana akiwa hoteli ya Kiwayu pwani ya Kenya.
Yeye pamoja na mumewe walikuwa wamewasili katika hoteli hiyo siku moja kabla ya kushambuliwa.Mama huyo alichukuliwa kwa mashua na watu walioshukiwa kuwa maharamia wa Kisomali.
Polisi wa Kenya wamesema watu sita waliokuwa wamejihami waliingia ndani ya chumba chao ambapo mumewe alipigwa risasi alipojaribu kuwakabili washambuliajo wao.
Kufuatia tukio hilo Uingereza iliwatuma polisi wake kusaidia katika uchunguzi.
Serikali ya mpito ya Somalia ilihusisha kundi la kiisilamu la Al shabaab kwa mauaji ya mtalii huyo na kutekwa nyara kwa mkewe. Hata hivyo kundi hilo limekanusha kuhusika na kisa hicho.