Na Waandishi Wetu
TAARIFA zilizotua kwenye dawati la gazeti hili kutoka nchini India juu ya hali ya mchekeshaji maarufu wa Kundi la Orijino Komedi, Joseph Shamba ‘Vengu’ zinatoa machozi kufuatia maelezo kwamba hali yake bado ni tete.
Mtanzania mmoja aishiye nchini humo anapotibiwa Vengu katika Hospitali ya Apollo, aliyejitambulisha kwa jina la Japhet Kris alilitumia gazeti hili barua-pepe akieleza kuwa, msanii huyo bado hali yake si shwari licha ya kwamba jitihada zinafanywa na madaktari kuokoa uhai wake.
“Nilipata fursa ya kwenda kumuona Vengu kwenye Hospitali ya Apollo, kwa kweli hali yake bado siyo nzuri ingawa kuna mabadiliko kidogo ya afya yake.
“Nilipomuona kwa kweli niliumia sana, nilikuwa na marafiki zangu Watanzania…tuliumia sana, hali yake inatia huruma sana kwa kweli.
“Nilijaribu kuzungumza na mmoja wa madaktari pale hospitalini akasema wanafanya wanavyoweza kuhakikisha anapona lakini kikubwa nawaomba Watanzania wenzangu walio huko nyumbani wazidishe maombi kwa Mungu hakuna linaloshindikana, atapona tu,” ilieleza sehemu ya ujumbe huo.
Ndugu wanasemaje?
Akizungumza na mwandishi wetu, ndugu mmoja wa Vengu aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa familia alisema: “Kuna ndugu yetu ambaye yuko kule anafuatilia kwa karibu matibabu yake (Vengu), juzi alitupigia simu na kutuambia kuwa amefanyiwa operesheni, kikubwa tuzidi kumuombea.”
Mama yake Vengu ana siri nzito
Huku kukiwa na madai kuwa mama yake, Bi. Hellen ana siri nzito juu ya
afya ya mwanaye, mambo ya kishirikina yakihusishwa, mama huyo alipatikana mwanzoni mwa wiki hii na kuelezea juu ya ishu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu Bi. Hellen alisema, kinachomsumbua mwanaye ni maradhi ya kawaida na wala siyo kwamba amerogwa kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodhani.
“Wapo wanaosema mwanangu amerogwa, ninachoamini ni kwamba anachougua Vengu ni maradhi ya kawaida hivyo wenye dhana hiyo potofu waachane nayo,” alisema mama huyo.
Ugonjwa wa Vengu
Mwishoni mwa mwaka jana, Vengu alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akikabiliwa na ugonjwa uitwayo kitaalam Brain au Cerebral Atrophy ambapo seli za kichwani hukosa mawasiliano na sehemu nyingine na mgonjwa kupoteza fahamu.
Hali ilipozidi kuwa tete, mchekeshaji huyo alipelekwa Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu zaidi.
0 Comments