Na Elvan Stambuli
 ADUI namba moja wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe ametajwa kuwa ni yule aliyevumisha na kusambaza ujumbe kwa watu mbalimbali kuwa kiongozi huyo amefariki dunia.
Chanzo chetu cha habari ambacho ni mmoja wa wanafamilia wa Dk. Mwakyembe kimeliambia gazeti hili kuwa adui huyo wa ndugu yao, familia inamjua lakini hivi sasa ni mapema mno kumtaja.
“Tunamjua tena ni mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi. Hatuwezi kumtaja kwa sasa lakini nakuhakikishia tunamjua,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, msemaji wa Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, Victor Mwambalaswa alimwambia mwandishi wetu kuwa ni kweli kuna mtu alizusha na kusambaza habari za kifo cha mpendwa wao.
“Hawa wanaoeneza uvumi huo wanasikitisha, kuishi au kufa ni mipango ya Mungu. Sijui anayeeneza hayo ana makusudi gani?” alihoji Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lupa.
Alisema Dk. Mwakyembe ni mzima wa afya na angezungumza na waandishi wa habari jana (Jumatatu) baada ya kurejea kutoka India mwishoni mwa wiki iliyopita.
Dk. Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9, mwaka jana yalimlazimu kupelekwa katika Hospitali ya Apollo, India kwa matibabu zaidi.
Maradhi hayo yamezua utata mkubwa baada ya kudaiwa kuwa yametokana na kulishwa sumu huku kukiwa na kauli zinazotofautiana kutoka kwake na baadhi ya watendaji wengine wa serikali.



Kauli tete ziliibuka baada ya baadhi ya viongozi akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kudai kuwa maradhi yanayomsumbua Dk. Mwakyembe yametokana na kulishwa sumu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alijibu madai hayo aliposema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Dk. Mwakyembe hajaugua kwa sababu ya kulishwa sumu bali ana maradhi ya ngozi na kutishia kuwachukulia hatua waliotoa kauli hizo.
Ripoti ya uchunguzi aliyoisoma Manumba katika mkutano wake na waandishi wa habari Februari 16, mwaka huu Dar es Salaam, inaonyesha kuwa Dk.Mwakyembe hakulishwa sumu huku akisema kwamba pia ulijumuisha taarifa kutoka hospitalini India ambako alikuwa anatibiwa.
Alisema uchunguzi huo unalipa jeshi la polisi picha kuwa waliotoa taarifa hizo hadharani wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baada ya kauli hiyo, Dk. Mwakyembe aliibuka na kutoa kauli nzito iliyoonekana kumjibu Kamishna Manumba akielezea kushangazwa kwake na majibu hayo na kudai kuwa hayakuwa sahihi.
Mbali ya Dk. Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa nyakati tofauti walikana kuijua ripoti hiyo ya Kamishna Manumba na kila wanapobanwa anamtupia ‘mzigo’ kachero huyo mkuu wa upelelezi nchini.
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kudhamiria kuchukua hatua, inadaiwa kuwa Kamishna Manumba aliwasilisha jalada la mashtaka kwa watu anaodai wanaeneza habari ya kulishwa sumu Mwakyembe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi ambaye alithibitisha kulipokea lakini akasema ni vigumu kufahamu ni lini atalipeleka mahakamani jalada la kesi hiyo.