Kundi la maseneta 33 wa Marekani wamewasilisha azimio la kulaani uasi wa kundi la Lord’s Resistance Army (LRA) na kiongozi wake Joseph Kony kwa maovu waliyoyafanya yakiwemo ubakaji, kukata watu viungo na kufanya mauaji ya kinyama.
Azimio hili linaunga mkono juhudi za jamii ya kimataifa ya kumaliza vitisho kutoka kwa kundi hili la waasi nchini Uganda.
Uungwaji mkono huu unatokana pia na kuongezwa kwa majeshi nchini Uganda kuwalinda raia na kusaidia pia katika kuwakamata wapiganaji wa LRA.
Mwezi wa Oktoba mwaka jana Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kupeleka wanajeshi 100 nchini Uganda kusaidia majeshi nchini humo kupambana na wapiganaji wa LRA.
Azimio hili la maseneta limekuja wakati ambapo filamu inayoshinikiza kukamatwa kwa kiongozi wa kundi hilo la waasi imepata umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii ya facebook na twitter na kuamsha hisia na kumbukumbu ya uasi huo miaka sita baada ya kumalizika kwake kaskazini mwa Uganda wakati Kony alipoondoka na kukimbilia katika mataifa jirani.