Pichani kulia Baba wa mtoto aliyekulia nje ya tumbo la uzazi la mama yake kwa miezi tisa akiwa na mwanae.
Hospitali ya Mikocheni ya jijini Dar es Salaam imemruhusu baba mzazi wa mtoto aliyekulia nje ya tumbo la uzazi la mama yake kwa miezi tisa kumchukua mtoto huyo na kumwahidi kumpatia huduma ya matibabu ya afya bure kwa miaka mitano.
Akizungumza na Chanzo cha habari hizi hospitalini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mikocheni, Dk. Asser Mchomvu, alisema kuwa wameamua kumruhusu baba mzazi wa mtoto huyo amchukue mtoto wake baada ya kulidhika na afya ya mtoto huyo aliyekuwepo hospitalini hapo kwa wiki mbili chini ya uangalizi wa madaktari.
“Tumemruhusu amchukue mtoto wake, baada ya kuona afya ya mtoto huyo inaendelea vizuri na atakuwa anatibiwa bure pasipo gharama zozote katika hospitali hii kwa kipindi cha miaka mitano kutoka sasa,” alisema.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Okolewa Amoni, alisema anaushukuru uongozi wa hospitali kwa msaada mkubwa walioutoa kwake.
Alisema kuwa, mtoto wake kupata huduma ya matibabu bure kwa miaka mitano ni msaada mkubwa kwake kutokana na mama mzazi wa mtoto huyo kufariki dunia.
Mwezi uliopita, jopo la madaktari bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Kairuki katika hospitali ya Mikocheni, walifanikiwa kuokoa maisha ya mtoto mchanga aliyekulia juu ya utumbo kwenye tumbo wa mamaye kwa miezi tisa, lakini mama yake alifariki kutokana na kutokwa na damu nyingi.