Donald Payne.
Mbunge wa kwanza mweusi kuchaguliwa katika bunge la Marekani kutoka katika jimbo la New Jersey ameaga dunia kutokana na saratani ya utumbo akiwa na umri wa miaka 77.
Wabunge wenzake na wanaharakati walimwelezea marehemu Payne wa chama cha Democratic aliyeaga dunia Jumanne kama mbunge aliyefanya jitihada kuwasaidia watu wa eneo alilowakilisha na wengine wengi waliokabiliwa na matatizo nje ya Marekani.
Kama mbunge katika baraza la wawakilishi la marekani, Payne alitaniwa kuwa balozi wa Afrika.
Alitetea mfuko wa fedha wa dola milioni mia moja kusaidia kuzuia na kudhibiti Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria hususan katika nchini za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.
Darius Mans , Rais wa shirika la Africare jijini Washington, alimweleza marehemu Payne kama mbunge aliyejali sana matatizo yanayokumba bara la Afrika. Mbunge Donald Payne alichaguliwa katika baraza la wawakilishi la bunge la Marekani mwaka wa 1988 akiwa mbunge wa kwanza Mmarekani mweusi kuchaguliwa katika jimbo la New Jersey.
Wabunge walielezea jinsi marehemu Payne alivyopigania misaada ya kibinadamu ipelekwe Darfur magharibi mwa Sudan ambapo kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mnamo mwaka wa 2009, Payne alinusurika shambulizi la kombora katika uwanja wa ndege mjini Mogadishu, Somalia. Ndege yake iliweza kuondoka bila tatizo. Alikuwa amemaliza ziara yake nchini humo baada ya kuzungumzia maswala ya kiulinzi na viongozi wa Somalia. Donald Payne atakumbukwa kama mtetezi wa haki kwa wote .
1 Comments