Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
Hakimu Mwafongo, Iringa
RAIS Jakaya Kikwete amewataka viongozi na wanasiasa wakiwamo wabunge na madiwani kuacha kusababisha migogoro kwa maslahi yao binafsi katika kusimamia maji ya Bonde la Mto Rufiji kwa lengo la kulinusuru bonde hilo.Pia Rais Kikwete ameagiza Mto Ruaha usimamiwe vizuri kwa sababu maji yamekauka na kuhatarisha uchumi wa taifa kwa kuwa unatumika kuzalisha umeme na chakula.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo baada ya kufanya ziara katika maeneo mbali mbali ikiwamo Pawaga unakopita Mto Ruaha na kuona jinsi maji yalivyopungua kwenye mto huo.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Iringa, Rais Kikwete alisema hakuna njia ya mkato kunusuru bonde hilo isipokuwa viongozi wa serikali kusimamia kiukamilifu.
“Wakati Serikali inapoamua kusimamia mazingira ikiwamo kuwaondoa watu kwenye vyanzo vya maji, wabunge na madiwani acheni kusababisha migogoro kwa maslahi yenu binafsi, acheni tamaa ya kuomba kura kwa kutumia bonde hili badala yake angalieni maslahi ya Taifa.
“Kama itatokea vita kuu ya tatu ya Dunia, basi itakuwa vita ya kupigania maji, hali imekuwa mbaya sana na hakuna njia ya kujinusuru zaidi ya kufanya mabadiliko tena haraka,” alisema Kikwete.
Alisema ikiwa maji yataendelea kupungua kwa kasi, uchumi wa taifa utayumba kwa kuwa Taifa linategemea bonde hilo kujiendesha kiuchumi na kuzalisha umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu sambamba na chakula kinachozalishwa kwenye mabonde Usangu, Kilombero na Rufiji.
“Itafika wakati chakula kitakuwa tabu, umeme shida na asilimia 80 mpaka 90 ya umeme na chakula nchini, kinapatikana katika Bonde la Ruaha, lazima tuchukue hatua za kulinusuru haraka bonde hilo,” alisema.
Kutokana na hali hiyo aliziagiza wizara zinazohusika kutafakari hatua za haraka ili kunusuru maji katika mabonde hayo.
Rais Kikwete alisema maji yamepungua nchini kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu mazingira kama vile kukata miti, kuchoma moto hovyo na kuishi karibu na vyanzo vya maji.
Alisema uharibifu huo umesababisha kuwapo kwa vipindi virefu vya tatizo la ukame na mafuriko.
Alisema kwa nchi zilizoendelea, suala la viwanda limekuwa likihatarisha amani ya nchi kutokana na kuwapo kwa mabadiliko makubwa ya tabia nchi.
“Wakubwa wanaochafua mazingira wamekuwa wabishi kuchukua hatua kunusuru mazingira, hali hii itaendelea kuwa mbaya zaidi kwa sababu tayari kina cha bahari kimepanda, joto limeongezeka na kipindi cha ukame kimeongezeka,” alisema Kikwete.
Alisema ipo haja kwa viongozi kusimamia kwa ukaribu suala la mazingira na upatikanaji wa maji ili kuweza kufikia malengo ya millennia ikiwemo suala la wananchi wote kufikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Rais Kikwete alizindua miradi mikubwa ya maji miwili Mkoani Iringa wa kwanza ukiwa wa maji safi na taka wa manispaa ambao umegharimu zaidi y ash Bil 73 na kuweza kufikisha asilimia 96 ya wananchi wote wanaopata huduma ya maji safi.
Mradi mwingine ni wa Pawaga ambao umefadhiliwa na kanisa la Aglikan na kughalimu zaidi ya sh Bil mbili, ambao umewafikia zaidi ya wananchi 20,500 wa maeneo hayo.
Aliwataka wananchi kutunza miradi hiyo ambayo imefadhiliwa na Jumuiya ya Watu wa Ulaya na Ujerumani ili kuepuka tatizo la upatikanaji wa maji ambalo lilidumu kwa muda mrefu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr Christine Ishengoma alisema mkoa huo umeanza kuhifadhi vyanzo vyake vya maji
0 Comments