Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bwana Ludovick Utouh akikabidhi ripoti yake kwa Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ikulu jijini Dar es Salaam jana asubuhi.Kushoto ni naibu mdhibiti n Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bwana Atanas Tarimo. Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jana, Alhamisi, Machi 29, 2012, amepokea rasmi Ripoti ya Mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Ludovic Utoah kwa mujibu wa mahitaji ya Kifungu 143 (4) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shughuli hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete kwa zaidi ya saa mbili amemsikiliza Bwana Utoh akiwasilisha Ripoti hiyo ya Mwaka wa Fedha wa 2010/2011 na ambayo zamu hii imepanuliwa kwa kiasi kikubwa kulingana na mahitaji ya sasa ya ukaguzi na ikilinganishwa na ripoti za miaka iliyopita.
Bwana Utoah amewasilisha Ripoti yenye sehemu mbili kuu ambazo ni (1) Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu na (2) Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa.
Mbali na ripoti hizo mbili kuu, Bwana Utoah pia amewasilisha Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma, Ripoti ya Ukaguzi wa Balozi wa Tanzania nje, Ripoti ya Miradi Mikubwa ya Maendeleo, Ripoti ya Ufanisi na Uchunguzi na Ripoti ya Ajali za Barabarani nchini.
Kwa kila ripoti, Rais Kikwete ametoa maelekezo ya usambazaji na hatimaye utekelezaji wa ripoti hizo kama ifuatavyo:
(a) Moja, Rais Kikwete ameagiza maandalizi kufanywa na ofisi yake ili kuwasilisha rasmi Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu kwa Waziri wa Fedha na kuwasilisha Ripoti ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya ripoti hizo kuwasilishwa rasmi Bungeni ili zijadiliwe na kutolewa ushauri kama ipasavyo.
(b) Pili, Rais Kikwete amemwelekeza Bwana Utoah kujiandaa ili aweze kuwasilisha hoja kuu zilizopo kwenye Ripoti hizo kwenye Baraza la Mawaziri ili washauri hao wakuu wa Rais waweze kujua kina nini kipo kwenye Ripoti hizo na yapi yanasemwa kuhusu Wizara mbali mbali
(c) Tatu, Rais amemwelekeza Bwana Utoah kuhakikisha kuwa Ripoti ya Hesabu za Serikali za Mitaa inawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa ALAT
(d) Nne, Rais Kikwete amewaelekeza Mawaziri na viongozi katika ngazi mbali mbali kuzipitia Ripoti zinazohusu maeneo yao ya kazi na kuzifanyika kazi kama ipasavyo.
Rais Kikwete amemshukuru Bwana Utoah na ofisi yake kwa kazi nzuri na kumtaka kuendelea na kasi hiyo kwa sababu kazi ya kufanya bado ni kubwa.
Rais amesema kuwa amefurahi kuona ofisi ya CAG imeanza kazi ya ukaguzi wa uchunguzi na ufanisi (forensic audit) kuhusu miradi mbali mbali ya maendeleo na shughuli nyingine zinazotumia fedha za umma.Mwisho.Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.Dar es Salaam
0 Comments