Na Sifael Paul na Imelda Mtema
Ile biashara haramu ya filamu za ngono kwa kutumia picha feki za mastaa wa Bongo kwenye ‘makava’ ya CD ili zipate soko nchini, imechukua kasi ya ajabu, Ijumaa lina ripoti kamili.
MASTAA WACHAFUKA MBELE YA JAMII
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa idadi kubwa ya mastaa wa Kibongo wamechafuka mbele ya jamii kutokana na wafanyabiashara hao kutumia picha zao bila ya ridhaa yao ili kujitajirisha.
Imebainika kuwa, wauzaji wa CD chafu wanaofanya biashara zao kwenye Mitaa ya Kongo, Shule ya Uhuru, Kariakoo, Magomeni, Ubungo na sehemu mbalimbali jijini Dar wamekuwa wakiwashawishi wateja kwa maelezo kuwa CD hizo zimechezwa na mastaa wanaoonekana kwenye makava.

BAADHI YA MASTAA WANAOTUMIKA
Baadhi ya mastaa wanaotumika katika makava hayo ni pamoja na waigizaji wenye majina makubwa kama vile Wema Isaac Sepetu, Aunt Ezekiel, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Richard Bezuidenhout, mkatanyonga Aisha Mbegu ‘Madinda’, mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ na mtangazaji wa runinga Bhoke Mgina.
Kwa mujibu wa wachuuzi wa mikanda hiyo ya ngono ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo hadharani bila kujali sheria, wameeleza kwamba ujanja huo wa kutumia picha za mtu maarufu wa Bongo, umewasidia kuongeza mauzo.
“ Mimi nilishawishika kununua CD hii ya ngono kwa bei kubwa kwa sababu niliiona picha ya Wema na muuzaji kunihakikishia kuwa imechezwa na yeye,” alisema Juma Kitwana ambaye aliingizwa mkenge na wauzaji hao.

PICHA ZA KUTENGENEZWA
Imebainika kuwa baadhi ya picha za mastaa zinazowekwa kwenye makava ya CD za ngono si halisi kwani zina sifa zote za kutengenezwa kwa njia ya kompyuta.
Imefahamika kuwa ndani ya CD hizo hakuna staa wa Kibongo hata mmoja badala yake kuna watu wengine ambao wanaonekana dhahiri kuwa ni wazoefu wa kucheza filamu za aina hiyo.


USHUHUDA WA MILLARD AYO
Mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo, naye kwa upande wake alikiri kununua muvi ya sampuli hiyo kwa Sh.10,000 maeneo ya Ubungo ambayo kwa nje iliandikwa ‘Wema Sepeto’ lakini alipokwenda kucheki akakuta kitu tofauti kama ilivyokuwa kwa nyingine zilizokuwa na makava ya Aunt, Lulu na Richard wa BBA.

IJUMAA LAZUNGUMZA NA MASTAA
Baada ya kupata mkasa huu wa kihalifu Ijumaa lilizungumza na baadhi ya mastaa hao ili kusikia maoni yao juu ya matumizi yasiyo halali ya picha zao ambapo kila mmoja alifunguka kivyake
WEMA
“Tayari nimetoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay Kinondoni (Dar). Watu wamekuwa wakiniambia juu ya kuonekana kwa CD hizo na kiukweli kabisa nikimkamata anayehusika lazima nimpandishe kizimbani,” alisema Wema.
AUNT
“Hao ni watu wenye tamaa ya utajiri wa haraka, lakini wanatudhalilisha sana kwa sababu wanatuchafua. Kiukweli wanatushushia heshima, hapa nasaka wakili tukifanikiwa kumkamata mmoja lazima nimchukulie hatua, siwezi kukubali kudhalilika bila sababu halafu mtu mwingine ajitajirishe,” alisema Aunt akionekana mwenye hasira.
LULU
“Kha! Hivi bado wanaendelea na biashara hiyo? Ukweli huo ni utapeli, wanapata fedha kwa njia ya uongo, mimi nikimbaini mtu anayefanya hivyo sitamuacha kwa sababu huo ni udhalilishaji uliopitiliza, mamlaka husika inapaswa kuingilia kati,” alisema Lulu.