KIZAZI kijacho huenda kisijue nini hasa maana ya Bagamoyo, mji uliokuwa na
barabara ya kwanza ya uhakika, mji wa kwanza makao makuu ya koloni la Kijerumani
na bandari ya kwanza kusafirisha pembe za ndovu na watu kama bidhaa.
Kwa
wale wanaopenda kuujua mji wa Bagamoyo katika mkoa wa Pwani, wataujua kwa namna
ambavyo wao wanapenda kuujua. Lakini, kwa wanazuoni na watafiti wa masuala ya
jamii na historia yao, ni dhahiri mji huu unatoweka katika mazingira yao kwa
spidi ya mwanga, ingawa wenyeji hawalioni hilo.
Nilipata bahati ya
kwenda Bagamoyo hivi karibuni. Nilifikishwa na waungwana pale kwenye Msalaba,
lakini niliporudi katika nyumba niliyofikia, niliwafikiria wote wanauzuru
Bagamoyo.
Naam, wanaozuru Bagamoyo wawe wale wa kidini, kihistoria au
kwa burudani, kitu kimoja kiwazi kabisa Bagamoyo mji wenye fursa na changamoto
za kimaendeleo, unakuwa mji wa kisasa, ukizima historia iliyopo polepole, na
mimi nathubutu kusema unakufa kihistoria,
wakazi wake hawana cha kujivunia.
Huhitaji tafakari kubwa ya kiprofesa, kujua kwamba hata katika Mji wa
Wafu, Kaole, uchakavu wake si wa kawaida na hata kama kunaonekana dalili za
kuhifadhiwa, upo ukweli kwamba hili ni tatizo.
Kizazi cha sasa hakiangalii sana uzima wa ukuukuu, unaostahili kuwapo katika
mji, ambao unakuwa bandari, unakuwa mji wa kufikia, unakuwa mji wa pilikapilika
za kisasa zaidi.
Mji huu wa zamani nchini Tanzania, wenye haiba ya aina
yake kihistoria, unakwenda pamoja na nyaraka nyingi kuonesha kwamba zipo juhudi
za kuhifadhi mji huo, ambao zamani ulikuwa maarufu kama kituo cha biashara na
mji wa kwanza wa watawala wa Kijerumani.
Ukitaka kujua kwamba mji huu wa
kihistoria unakufa ndani ya historia, maana ya Bagamoyo inateleza katika mdomo
tu, lakini maboma yale pasi shaka yanatoweka na vidatu vya kuingilia baharini,
pia zinatoweka na alama za njia, pia zinatoweka na mabaki ya maboma pia
yanatoweka.
Ruksa za ujenzi hazizingatii historia, inayoonesha kuwa
Bagamoyo kilikuwa kituo kikuu cha kibiashara, japokuwa biashara ya watu kama
bidhaa ilikomeshwa duniani mwaka 1873 na kuendelea karne yote ya 19, kwamba
wamisironari wa kwanza walifika hapo na kuchomeka msalaba, eneo ambalo linabanwa
na mahoteli na kwamba wajerumani walitengeneza boma lao la kwanza la kiutawala
pale.
Majani yanayoota hovyo, hayaoneshi uzuri wa historia na maswali kuwa kisima cha
kwanza
kilikuwa wapi, si rahisi kujibika. Usasa? Bagamoyo ambao upo kilomita
takribani 65 kutoka Dar es Salaam katika mazingira ya kawaida, si mbali vya
kutosha kutofanya maisha ya starehe kwa wakazi wake.
Lakini, pamoja na
umbali huo hafifu wa Bagamoyo inaonekana kuchakaa kwa kasi na kuchusha, si kwa
umaridadi wa sasa, bali kukosekana kwa ukarabati wa majengo ya zamani na
miundombinu ya zamani kuweka historia kama zamani.
Nuru ya maendeleo ya
kisasa kwa wakazi wanaoonekana kuwa na shida zaidi pengine kuliko ukubwa wa mji
na jina lao, Bagamoyo imekosa mvuto wa kihistoria kwa wananchi wake na majengo
yaliyobaki kuelezea Bagamoyo haitoshi kufikisha ujumbe stahiki kwa mji wa Kwanza
ulionakshiwa na historia ya Waarabu, Wajerumani na wamisionari.
Bagamoyo
jina kubwa tangu wakati wa utawala wa kiarabu, utawala wa Kijerumani na hata kwa
waingereza, sasa umeongezwa umaarufu zaidi kwa kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya
Kikwete, anatoka katika mji huo, lakini hata kwa wale wanaotengeneza zana za
sanaa pale penye picha nyingi za watu maarufu, unaweza kujiuliza inawezekana kwa
muda gani!
Utajiri mkubwa unaostahili Bagamoyo wa utalii - uwe wa ndani
au nje, haujaonesha kama utaweza kuwapo kwa miaka mingi ijayo na kusaidia
wananchi wa hapa, ambao ama hakika walistahili kujivuna.
Fikira za sekta
ya utalii kumeremetesha historia ya wenyeji wa Bagamoyo, zinazongwa na
ujenzi wa mahoteli ambao kwa namna ya tafakari ya karibu, yanachukua usasa
zaidi na kuendekeza utalii wa kwenye fukwe kuliko kusoma historia na makazi ya
zamani.
Kwa Adamu Mponda (29) ambaye pia ni mkazi wa Bagamoyo, mabadiliko yanayotokea,
yanaongeza shida zaidi badala ya kupata njia ya kutanzua yaliyopo, kwa
kuelimisha maana ya kutunza kila kitu kilichokuwapo hapo kale kwa manufaa ya
vizazi vijavyo.
Mawazo ya kuwapo kwa utalii, yamewezesha kuwapo kwa
ujenzi wa mahoteli, lakini mahoteli hayo yanasaidia nini katika hifadhi ya jina
na mambo yanayogusa Bagamoyo?
Viwanda vingi vinafikiriwa, maeneo ambayo
ni ya wenyeji na yenye historia za aina yake, nayo yanauzwa na wenyeji hao na
hakuonekani kama kuna juhudi zozote zile za kuhifadhi maeneo, si tu ya wakoloni,
lakini hata yale ya tambiko.
Ukiuliza maswali ni bajeti kiasi gani,
inatengwa kuhifadhi na kununua maeneo yanayostahili kuhifadhi ili kusiwepo na
uharibifu wa kihistoria, kama majengo yanavyovunjwa Dar es Salaam kwa neno la
usasa na kuondoa hatari kwa maisha ya wakazi wa majengo hayo,
Bagamoyo nako
vivyo hivyo.
Wakati wenzetu wazungu, hupiga picha majengo hayo na
kumwelekeza mtu ajenge kwa namna
ile ile, lililopokuwapo jengo, sisi
tunafuta historia kabisa. Je, watu zamani kabla ya kuendelea
na safari
walikula nini, mashamba yao yalikuwa wapi? Leo ukiuliza, huwezi kupata hata hilo
jibu la njia za mzunguko za kufikia bandarini kutoka kwenye boma na soko.
Pamoja na ukweli kuwa Bagamoyo haineemeki na kuwa historia ya kuwa makao
makuu ya Ujerumani, kituo cha biashara enzi za watumwa na mipango miji ya kwanza
kwa Tanganyika, Bagamoyo haionekani kuwa na mipango endelevu ya kutunza
rasilimali, ambayo ni mbegu ya utajiri wa elimu wa tabia za wananchi na athari
za biashara za watu katika mji huo.
Pamoja na fukwe nzuri, Bagamoyo ni eneo muhimu kwa kitamaduni, pwani na kitovu
cha makutano wa kitalii kwa pwani ya Tanzania. Ni dhahiri kuna changamoto za
kijamii katika kutunza uasili wa mji wa Bagamoyo, changamoto ambazo baadaye
zitanyima hata hao watalii
kidogo, wanaofika sasa kufuatilia mambo
mbalimbali.
Kama vile kuleta watalii bila kubadilisha utamaduni na
kutumia sekta kwa ajili ya maendeleo ni kitu kisichoonekana.
Watu kama
Yusufu (22) ambaye ni machinga katika eneo Msalabani, akiwa anauza kazi za
mikono (sanaa), wana wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu wanunuzi wengi wa kazi
hizo ni wazungu (watalii), ambao katika mazingira ya sasa ya kutohifadhiwa kwa
mji, kuwezesha utalii wa kale na yeye hatakuwa na kitu cha kuuza.
Ras T
ambaye anamiliki studio kwa ajili ya sanaa, akitoa maoni yake, anasema anadhani
serikali imeshindwa namna ya kuusaidia umma wa Bagamoyo, japo wapo katika
mazingira yenye mvuto mkubwa wa kujumuishwa na maeneo mengine nchini.
Mji wa Bagamoyo mwaka huu una ugeni mkubwa, unaotokana na historia yake.
Thamani ya mji huu ni kubwa hadi umepewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu
wa 20 wa Shirika la Ukasisi la Holy Ghost (Wamisionari wa Roho Mtakatifu) la
Kanisa Katoliki.
Ugeni huo utajumuisha wajumbe 115 kutoka duniani kote.
Hosteli ya Stella Maries mjini
Bagamoyo inaonesha historia ya mji ambapo
lilizaliwa Kanisa Katoliki katika Afrika Mashariki mwaka 1868.
Ni
heshima kubwa kwetu sisi kama taifa, kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kiasi hiki
na wenye heshima kubwa. Lakini, kwa spidi hii ya kutokuwa na mpangilio mahsusi
kuhusu Bagamoyo, mpangilio ambao utalinda hadhi ya mji au la, kwa kuangalia bila
kujali makaratasi
yenye mipangilio isiyofanyiwa kazi, Bagamoyo inakufa.
0 Comments