MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga, wametua salama jijini Cairo, Misri tayari kuwavaa wapinzani wao, Zamalek leo saa 12 jioni ya huko sawa na saa moja usiku, hapa nyumbani.
Msafara wa Yanga uliwasili jijini humo juzi asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri na maofisa wa ubalozi wa Tanzania waliwapokea chini ya ulinzi wa uhakika na mara moja wakawapeleka katika hoteli waliyopangiwa.
Mara baada ya kufika kwenye hoteli hiyo, kulizuka hali ya mabishano makali baada ya viongozi walioongozana na timu hiyo kubaini wamepangiwa kwenye hoteli ya kiwango cha chini sana. Pamoja na kulalamika, hawakuwa na ujanja zaidi ya kuanza maisha.
Ofisa mmoja wa ubalozi, amelalamika kuwa kutokana na kutokuwa na mawasiliano ya kutosha, ubalozi usingejua kama Yanga imefikishiwa kwenye hoteli hiyo ya kiwango cha chini kabisa.
“Kuna hoteli zipo Kariakoo (Dar es Salaam) ni bora kuliko hii waliyofikia Yanga, wametushangaza sana. Lakini hawakutaka mawasiliano. Unajua Yanga wanajisahau, hapa wanawakilisha nchi hivyo walipaswa kutuambia vitu vingi.
“Kitu kibaya zaidi, hii hoteli inatazamana kabisa na Klabu ya Zamalek, kitu ambacho si sahihi,” alisema ofisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
“Ila tumeomba tukutane nao jana (juzi) jioni kwa ajili ya kujadili masuala kadhaa muhimu kwa ajili ya kuwasaidia nini cha kufanya hata kama muda umeshatutupa mkono.”
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu, alithibitisha kutua salama kwa timu hiyo.
“Kweli wamefika salama na kupokelewa na maofisa wa ubalozi wa Tanzania. Tunasubiri taarifa kamili kujua kinachoendelea, ila wamelalamika tu kuwa baridi ni kali.”
Katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Februari 18 jijini Dar es Salaam, Yanga ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Zamalek, hivyo inaweza kusonga mbele iwapo itashinda au kutoka sare inayoanzia mabao mawili.
0 Comments