Na Wilbert Molandi
BAADA ya kufanikiwa kuingia katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kwa kuwaondoa wapinzani wao, ES Setif ya Algeria, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amewashukuru mashabiki wa Yanga.
Simba imefanikiwa kutinga katika hatua ya 16 bora na inatarajiwa kukutana na Al-Ahly ya Sudan katika mchezo utakaochezwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana kati ya Mei 11, 12 au 13 nchini Sudan.
Kufuatia ushindi huo, Rage ameliambia gazeti hili kuwa, ameshangazwa na ushirikiano walioupata kutoka kwa Watanzania waishio Algeria ambao wengi ni mashabiki wa Yanga.
Alisema mashabiki hao walichangia kwa kiasi kikubwa timu yake kupata matokeo mazuri kutokana na sapoti kubwa waliyokuwa wakiitoa tangu wafike kwenye Mji wa Setif.
“Tunawashukuru sana mashabiki wa Yanga waishio Algeria, wamechangia kwa kiasi kikubwa sisi kupata matokeo mazuri.
“Tulishangaa kwa mara ya kwanza mashabiki hao walifika hotelini wakiwa na kadi zao za uanachama walizozionyesha, wameonyesha uzalendo mkubwa kwa manufaa ya taifa na huu uwe mfano tunapofika katika michuano ya kimataifa,” alisema Rage.