BUNGE la Muungano lililomaliza kikao chake cha kumi jana, lilitikisika baada ya kuibuka kwa tuhuma nyingine nzito zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na naibu wake, Adamu Malima, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Wakati Ngeleja akishambuliwa kwa kusema uongo na kuficha ufisadi wa kutisha wa ubinafsishaji, Waziri Maige amekaangwa kwa tuhuma za kujihusisha katika ugawaji vitalu vya uwindaji kinyume na sheria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James lembeli, ndiye aliyeibua tuhuma hizo nzito, kiasi cha kuitaka serikali kumwajibisha waziri huyo, hatua ambayo imezidi kuonyesha uozo wa utendaji ndani ya serikali.
Lembeli akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha Aprili, 2011 hadi Aprili 2012, alisema uchunguzi wa kamati hiyo umebaini mchakato wa ugawaji vitalu ulikuwa na dosari nyingi ikiwamo waziri kutangaza majina ya waliopatiwa vitalu bila kuonyesha ni vitalu gani na vingapi walivyopewa.
Alisema baadhi ya kampuni ziligawawa vitalu kinyume na sheria na ushauri wa kamati ya kumshauri waziri kulingana na sifa na vigezo ikiwamo makampuni matatu, Mwanauta and company Ltd, Saidi Kawawa Hunting Ltd na Malagalasi Hunting Safaris Ltd kugawiwa vitalu bila kuwa na sifa.
Lembeli alisema kamati ilibani kampuni 16 ziligawiwa vitalu vya daraja la kwanza na la pili ambavyo havikuombwa wakati kulikuwa na kampuni za kizalendo zilizokuwa na vigezo.
“Dosari hizi ziliathiri dhana ya uwazi na utawala bora, na kuashiria kuwapo kwa rushwa katika zoezi hilo na hivyo kusababisha malalamiko makubwa kutoka kwa waombaji.
“Kamati ya Bunge inapendekeza kwamba Bunge liitake serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, kwa kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuyanyang’anya makampuni 16 vitalu vilivyogawiwa,” alisema.
Kuhusu usafirishaji wanyama nje bila kufuata taratibu, Lembeli alisema kamati hiyo imependekeza Bunge liiagize serikali kuwachukulia hatua kali za kinidhamu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ladislaus Komba, na wale wote waliohusika na utoaji wa vibali hivyo.

Aliitaja kampuni ya Jungle International kuwa moja ya zilizopewa leseni wakati kwa mujibu wa taarifa za Msajili wa Makampuni (BRELA), haipo kihalali na wala haikupeleka maombi ya kupewa wanyama hao.
Alisema waligundua kuwa kibali alichopewa Jungle International kilielezea ukamataji wa wanyama kufanyika katika wilaya za Longido, Simanjiro na Monduli, jambo ambalo ni kinyume na kanuni, kwani kibali lazima kiainishe wilaya moja.
Aidha alisema kampuni ya Jungle si kampuni halali ya kuendesha biashara ya wanyamapori, kwani Desemba 28, 2001 ilibadili jina la shughuli zake na kwa sasa imesajiliwa kwa jina la Jungle Auctioneers & Brokers Company ambayo inafanya shughuli za udalali.
“Kwa msingi huo, wizara kupitia barua kumbukumbu namba GD/T.80/85/98 ya Aprili 29, 2011 iliyosainiwa na M. Madehele kwa niaba ya Katibu Mkuu ilitoa kibali kwa kampuni ambayo haipo. Hali hiyo inadhihirisha udanyanyifu wa kutisha, harufu ya rushwa na uhujumu uchumi wa nchi,” alisema.
Aidha kamati hiyo imebaini kuwa Kamran Ahmed, raia wa Pakistan ambaye mwaka 2009 alijitambulisha kwenye Idara ya Wanyamapori kama mwakilishi wa Serikali ya Jiji la Karachi aliingia mkataba na aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Erasmus Tarimo kwa niaba ya serikali na kusafirisha tembo wanne kinyume cha sheria.
Alisema kamati hiyo ilifanya uchunguzi zaidi na kubaini Julai 19, 2010, wizara hiyo ilitoa kibali kilichosainiwa na B.M.C.M Midala kwa niaba ya serikali ya Katibu Mkuu wa Serikali ya Jiji la Karachi kuruhusu usafirishwaji wa twiga wawili, viboko (2), greater kudu (2) na errands (4).
“Kwa ushahidi uliopo katika kikosi dhidi ya majangili, Arusha, raia huyo wa Pakistan aliyepewa kadi ya ukamataji wanyamapori 0016929 aliwahi kuwa na kesi nyingi za kujihusisha na ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hao kinyume na sheria,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema kamati hiyo imeshashauri Tarimo, Ahmed na wengine waliohusika katika sakata hilo wachukuliwe hatua stahiki.
Hata hivyo, kamati ilieleza kukabiliwa na changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka wizarani hasa walipohitaji baadhi ya nyaraka muhimu kama barua halisi ya Jungle International kuomba kupatiwa wanyama na barua halisi ya serikali ya Jiji la Karachi kuomba kupatiwa tembo wanne na kumtambulisha Ahmed kama mwakilishi wake kwa Idara ya Wanyamapori nchini.
Zitto awashukia Ngeleja, Malima
Kwa upande wa Ngeleja, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) Kabwe Zitto (CHADEMA) alimshambulia waziri huyo na Naibu wake Adamu Malima kwa madai ya kusema uongo kuhusiana na uwekezaji katika mgodi wa Kiwira.
Zitto akitoa taarifa kwa Bunge kutokana na jibu la Ngeleja aliyedai kuwa kampuni ya Tanpower Resources kwa sasa ni mfilisi baada ya kushindwa kuendeleza uwekezaji katika mgodi wa Kiwira na ikaurudisha serikalini na imelazimika kuhamisha umiliki wa Mlima Kagulu ambao unasadikiwa kuwa na mashapo yapatayo tani milioni 80 za makaa ya mawe kwenda kwa kampuni ya Tanzacoal kwa kufuata taratibu zote za kisheria.
Mlima huo wenye hazina kubwa ya makaa ya mawe ndiyo tegemeo la mwekezaji ambaye atamilikishwa Kiwira kuchimba makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha megawati 400 za umeme.
Zitto alisema kuwa Mlima Kagulu uliokuwa unamilikiwa na Shirika la Madini (Stamico) ulimilikishwa kwa Tanpower Resource kwa maagizo ya aliyekuwa Waziri wa Nishati wa wakati huo ambaye pamoja na kutomtaja jina lakini alikuwa ni Daniel Yona.
Zitto alidai kuwa waziri huyo ndiye aliyeiagiza Stamico isiombe tena leseni ya kumiliki mlima huo wenye utajiri wa makaa ya mawe badala yake akaipa kampuni ya Tanpower Resources ambayo alikuwa na hisa nayo.
Alisema kampuni hiyo haikufuata utaratibu wa kumilikishwa mlima huo kwa mwekezaji mwingine, wakati imeingizia madeni makubwa serikali yafikiayo sh bilioni 33 ambazo zilikopwa na wawekezaji hao kutoka benki mbalimbali ambapo kwa sasa zinalipwa na serikali.
Zitto aliongeza kuwa licha ya hasara iliyosababishwa na Tanpower Resources, lakini serikali imelazimika kuilipa kampuni hiyo sh bilioni 9 kama ada ya kuendesha menejimenti ya mgodi huo jambo alilosema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria.
“Kwa hali hii serikali iwajibike juu ya suala hili,” alisema Zitto kauli iliyomfanya Spika wa Bunge Anne Makinda kumtaka mbunge huyo kuwasilisha hoja hiyo kwa maandishi ili serikali kwa hoja yake ilikuwa nzito na ambayo lazima serikali itoa maelezo.
Wabunge wamtetea Waziri Nyalandu
KATIKA hatua isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri wamemuunga mkono Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyalandu, kuhusu sakata la Shirika la Viwango Nchini TBS.
Aidha wabunge hao wameshauri kwamba hoja inayoendelea hivi sasa kuhusu taarifa ya utendaji ya TBS na mapungufu yake isitumike vibaya kuwahujumu wanasiasa wengine badala yake wanaohusika wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa mapendekezo yaliyopo.
Wakizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima nje ya viwanja vya Bunge mjini hapa wabunge hao walisema taarifa hizo zinapaswa kufanyiwa kazi kikamilifu kwani zinaweza kuwaweka baadhi ya wanasiasa wakiwamo mawaziri katika hali tete.
“Tunaelewa kwamba katika hili ni nani anayetakiwa kuwajibishwa, lakini kumekuwa na maoni tofauti ambayo kwa utashi wa kawaida wa kisiasa, wanafanyiwa fitina ili kumshawishi Mheshimiwa Rais kuwaondoa,” alisema mmoja wa wabunge hao kutoka kanda ya ziwa.
Wabunge hao ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini walisema mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya Wabunge wa CCM hayakuwataja baadhi ya mawaziri, lakini wameshangazwa kuona majina yao yakiunganishwa katika sakata hilo hatua ambayo inaweza kutafsiriwa vibaya na jamii.
“Tumekuwa katika vikao vya chama na mapendekezo yalikuwa ya wazi, hivyo haikuwa hoja ya msingi kuingiza majina ya baadhi ya mawaziri na tunadhani kwamba hatua hii inafanywa kwa makusudi na wala sio bahati mbaya,” alisema mbunge mwingine.
Mbunge huyo alisema binafsi hatoi maoni yake kwa nia ya kumtetea Naibu Waziri Nyalandu, bali anafanya hivyo ili kuonyesha uzalendo kwa taifa hili na kama kuna makosa mengine ameyafanya, anaweza kuwajibishwa lakini sio kwa hilo la TBS.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kamati ya Bunge pamoja na ile ya CCM ilitoa ushauri kwamba Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami awajibishwe kutokana na kushindwa kuchukua hatua kulingana na mamlaka aliyopewa na sheria.
Walisema kwamba mfumo wa utendaji katika idara za serikali unatambua nafasi ya Waziri na Naibu Waziri, hivyo suala linalomhusu waziri kamwe haliwezi kuchukua nafasi ya Naibu Waziri kutokana na uzito wa jambo husika.
“Ndio maana hata katika vikao vya uchambuzi wa taarifa za kamati, suala hili tumelisemea kwa kiasi kikubwa na kuweka msimamo kuwa anayetakiwa kuwajibika kwa kushindwa kulifanyia maamuzi ni Waziri mwenye dhamana na wala sio mtu mwingine,” alisema mbunge mwingine.
Mbunge huyo alisema ikiwa Watanzania wataendelea kupewa taarifa zisizo za kweli watashindwa kuiamini serikali, lakini pia watakuwa wamewekewa chuki za kisiasa moyoni dhidi ya baadhi ya mawaziri waliopo madarakani na kusema mfumo wa sasa unaingilia mamlaka nyingine za uteuzi kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Tunakubali kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wameshindwa kusimamia majukumu waliyopewa na Rais ama wamechoka au kulewa madaraka, hivyo ni muhimu kuchukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wasioweza kufanya majukumu kwa mujibu wa taratibu zao,” alisema mbunge mwingine.
Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami, alisema kwa sasa hawezi kusema chochote kwa vile yupo kwenye msiba mjini Moshi.
“Samahani ndugu yangu, niko Moshi nimefiwa, hivyo sitakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo, nakuomba ufanye subira kwani Waziri Mkuu anaweza kulitolea ufafanuzi suala hilo wiki hii,” alisema Chami.
Wabunge bado walia na mawaziri
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu ‘Sugu’, alisema taifa limepoteza fedha nyingi kutokana na uzembe wa mawaziri na kuhoji wanyama kama twiga waliosafirishwa walitumia usafiri gani.
“Hata kama mnasema hamtajiuzulu, hiki kimbunga ni lazima king’oe bati ambalo ni Mheshimiwa Pinda. Huu sio upepo ni dhoruba nasema kama mmeshindwa achieni ngazi sisi tushike madaraka, kama tunatoa bajeti mbadala na inakubaliwa kwa asilimia 99 tunaweza,” alisema.
Aliongeza kuwa hata CCM ikiwa chama pinzani hawataki kiwe legelege na kuongeza kuwa ndiyo maana wakati huu wanawanyoosha.
Pamoja na hayo, Sugu alisema endapo wangekuwa wanafuata hasira za wananchi, viti vya bungeni vingekuwa vimeshang’olewa siku nyingi.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), alisema mawaziri wanaogoma kujiuzulu ni lazima wajiuzulu, kwani lazima inakuja tsumani katika suala hilo.
Alisema ni mambo ya kushangaza kila mwaka yanazungumza masuala hayohayo, lakini hakuna kinachobadilika na kuongeza kuwa vizazi vijavyo vitakuja kuwalaumu.
“Wabunge tunapoibua masuala haya naona mawaziri wanaona ni mzaha, kwani mjadala uliopoanza Waziri Maige ametoka nje ya ukumbi wa Bunge.
“Kule KIA (Kilimanjaro International Airport) vijana wanalalamika kuwa kuna baadhi ya watu wanaokuja kugongewa passport zao huku wenyewe wakiwa kwenye ndege,” alisema.
Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (NCCR-Mageuzi), alisema kutokana na hali inayoendelea serikalini ndiyo maana wanawataka mawaziri hao kujiuzulu kutokana na kuihujumu nchi.
Alisema ni jambo la kushangaza kampuni kupatiwa vibali bila kuomba na kuongeza kuwa viongozi wa CCM ndio wanaoiangusha serikali yao.
“Jamani hii nchi ni ya aina gani, ni kitu gani mnafanya? Tuwaelewaje? Hivi mnatuona wapinzani ni nyanya mbichi?...mheshimiwa Spika funga mlango tushikane mashati,” alisema.