CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juzi ya kumvua ubunge, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.

Uamuzi huo wa Chadema ulitangazwa katika mkutano mkubwa na wa aina yake wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya NMC mjini hapa ukihudhuriwa na umati wa wananchi wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema chama hicho kitakwenda mahakamani kupinga hukumu hiyo baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya Jaji Gabriel Rwakibarila aliyetoa hukumu hiyo. Mbowe alisema sasa Chadema itawasilisha rufaa yake Mahakama ya Rufaa ili kesi hiyo sasa iweze kupitiwa na kuamuriwa na jopo la majaji watatu na si mmoja kama ilivyokuwa awali.

“Maamuzi ya Jaji Rwakibarila hayakuwa sahihi na ni maamuzi ya kushangaza na yenye shinikizo ndio maana tumeona tukate rufaa ili kutafuta haki zaidi,” alisema Mbowe. Alisema sababu nyingine inayoifanya Chadema kukata rufaa ni kutokana na kutaka kuokoa fedha zaidi ya Sh bilioni 3 na milioni 300 za wananchi walalahoi walipa kodi ambazo zitatumika katika uchaguzi mdogo, badala ya kupelekwa kwa wananchi kushughulikia kero za afya, maji na huduma nyingine muhimu.

“Kama CCM (Chama Cha Mapinduzi) wamefurahi kwa kudhani kwamba wanakwenda kwenye uchaguzi mdogo, sisi Chadema tunasema hatuko tayari kwa hilo.Tuna taarifa kwamba Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imetia shinikizo kutolewa kwa hukumu hii.

“Serikali na Rais Kikwete wanapaswa kujua nchi inaongozwa na mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Mahakama na Dola. Kama Rais na Serikali wanaweza kuingilia uhuru wa Mahakama, basi tunasubiri Mahakama ya Rufaa itoe uamuzi wa rufaa,” alisema Mbowe.



“Tungeweza kukubali kwenda kwenye uchaguzi kwa sababu tuna imani ya kushinda kwa kishindo kwa mara nyingine lakini tukifanya hivyo CCM itapata mwanya wa kuingilia Uhuru wa Mahakama kwa kesi zingine za wabunge wa Chadema za Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) na John Mnyika (Mbunge wa Ubungo),” alisema Mbowe.

Kwa upande wake akihutubia umati huo, Lema aliwasihi wananchi kutokata tamaa na badala yake kuendeleza mapambano ili haki iweze kupatikana.
Alisema Jumanne ijayo ataandika barua kwenda kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kumtaarifu kwamba bado ni Mbunge wa Arusha Mjini lakini yupo likizo akisubiri kuamriwa kwa rufaa yake na Mahakama ya Rufaa.

Aliwataka wananchi wa Arusha Mjini na wapenzi wa Chadema kumuomba Mungu kwa kufunga kula chakula kwa muda wa siku saba ili Mungu aweze kuonesha maajabu yake.

Alisema kuanzia wiki ijayo Chadema itamtumia kwenda mikoa mbalimbali kuimarisha chama hicho na kujigamba kwamba nguvu yake itamwathiri Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole – Sendeka ambao alisema watang’olewa na wagombea wa Chadema katika uchaguzi mkuu ujao.

Pamoja na Chadema kukata rufaa, hukumu ya Mahakama Kuu ya kumpokonya Lema ubunge itaendelea kutekelezwa ili kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa inayoweza ama kukazia hukumu ya Mahakama Kuu au kumrejeshea ubunge.

Alipopata nafasi ya kuhutubia umati huo, Mbunge mteule wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema CCM wamekuwa wakihofia ushawishi wa Lema katika siasa lakini akasema kuingia kwake bungeni ni moto zaidi ya uliokuwa unaoneshwa na Lema.

Alimtaka Spika wa Bunge kufahamu fika kuwa Mbunge aliyeingia bungeni sasa ni Mbunge machachari zaidi kuliko ilivyo kwa Lema ajiandae kupambana na hoja atakazozitoa kwa nia ya kuwatetea wananchi wanyonge na masikini.

Umati mkubwa wa wananchi ulifurika kwenye viwanja hivyo ili kuwasikiliza viongozi hao wa Chadema Taifa, huku wengi wao wakiwa na mabango yenye ujumbe wa maneno mbalimbali yakiionya Mahakama, Serikali na Polisi kuacha kuingilia maamuzi ya wananchi.