Inafahamika kuwa Pep Guardiola anakaribia kuacha kuifundisha Barcelona baada ya kuifahamisha klabu hiyo kuwa hawezi kuendelea kuwa kocha.
Guardiola mwenye umri wa miaka 41 atatangaza nia yake hiyo katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa alasiri.
Iwapo hatobadili mawazo yake, Guardiola anatarajiwa kuthibitisha habari za kuondoka katika timu aliyoipa ushindi wa Klabu Bingwa Ulaya mara mbili. Meneja huyo amepanga kukutana na wachezaji asubuhi ya Ijumaa.
Inadhaniwa kuwa Guardiola atachukua mapumziko ya mwaka mmoja kufundisha soka, iwapo atatangaza uamuzi wa kuacha nafasi yake hiyo.
Guardiola alikutana na rais wa Barcelona Sandro Rossell kwa muda wa saa tatu siku ya Alhamisi asubuhi.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Rossell mjini Barcelona, Guardiola anasemekana alionesha kuwa "hawezi kuendelea tena".
Mazungumzo yaliyoanza kuhusu kuongeza mkataba wake wa kila mwaka, kwa mwaka mmoja, yalibadilika na kuwa ya kumshawishi asiondoke kabisa. Inafahamika kuwa Rossell amempa Guardiola uwezo wa kutumia kiwango anachotaka kusajili, lakini kocha huyo hakuchukua uamuzi wake kuhusiana na fedha.
Guardiola ambaye alikuwa nahodha wa Barcelona wakati akicheza soka, amekuwa akisisitiza kuwa atafanya kila awezalo kusaidia klabu hiyo. Alitumia siku ya alhamisi mchana akiwa na familia yake na anatarajiwa kumwambia Rossell uamizi wake baadaye usiku.
Wakati uwezekano wake wa kubadili mawazo bado upo, klabu hiyo ina wasiwasi kuwa mtu aliyewaongoza kunyakua makombe mawili ya Klabu Bingwa Ulaya na vikombe vitatu vya ligi kuu huenda amekwisha fanya uamuzi wake.
Jinsi Barca walivyofungwa na Real Madrid siku ya Jumamosi, matokeo ambayo yalididimiza matumaini ya kuchukua uningwa wa ligi kuu na pia kutolewa na Chelsea katika Klabu Bingwa Ulaya ndio kumesababisha uamuzi wake huo
0 Comments