WAKATI Wakristo Watanzania wakiungana na wenzao kote duniani kuadhimisha sikukuu ya Pasaka jana, majambazi wamevamia makazi ya viongozi wa dini ya Kikristo katika Parokia ya Nyangao wilayani Lindi mkoani Lindi na kuwajeruhi viongozi wawili na kupora fedha.

Majambazi wapatao 10 walivamia makazi hayo usiku wa saa 6.45 wa Alhamisi iliyopita na
kuwajeruhi watu wanne, wakiwamo viongozi wawili wa dini parokia hiyo na kupora fedha zaidi
ya Sh milioni tano.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Mwakajinga alisema watu watatu kati ya hao, walishambuliwa kwa kupigwa mapanga sehemu mwilini wakati mmoja alifungwa kamba na kutupwa kwenye shimo la taka.

Mwakajinga aliwataja walioshambuliwa kuwa ni Paroko Housiager Hugo (74), Padri Michael
Mrope (75) pamoja na walinzi wawili wa nyumba hiyo, Victor Hanga (58) na Joseph Mathias (45).
Alisema Hugo, ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Misheni ya Ndanda iliyopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, amepigwa mapanga kichwani na mbavuni, ambapo Hanga ambaye ni mlinzi, amejeruhiwa pia kwa panga kichwani na kulazwa Hospitali Teule ya Nyangao.

Aidha, alisema Padri Mrope alishambuliwa kwa kupigwa wakati mlinzi wake alifungwa kamba na kutupwa kwenye shimo la taka hadi majambazi hao walipoondoka na kuokolewa na Polisi waliofika kwenye eneo hilo.

Alisema majambazi hao zaidi ya 10 walikuwa na silaha mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na bunduki, walivamia makazi ya viongozi hao na kupora fedha taslimu kiasi cha Sh milioni tano na kutokomea zao.



“Kabla hawajazichukua fedha hizo, walipambana na walinzi waliokuwa wakiwalinda, lakini
walizidiwa nguvu na ndipo majambazi hao walimfunga kamba mlinzi mmoja na mwingine kumjeruhi kwa panga kichwani,” alisema Kaimu Kamanda wa Polisi.

Alisema katika tukio hilo, hakuna mtu aliyekwisha kamatwa hadi sasa na kwamba askari wanaendelea na kazi ya kuwasaka majambazi hao ili yachukuliwe hatua za kisheria, ikiwamo kuwafikisha mahakamani.

Katika hatua nyingine, maaskofu na mapadri nchini wamewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa Tume ya Kukusanya maoni na Kuratibu mchakato wa Katiba, huku ikionya kuwa nchi inaelekea pabaya kutokana na baadhi ya watu kuamini kuwa haiwezekani kufanya siasa bila kugombana.
Akihubiri katika Ibada ya Pasaka jana katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam, Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa ameonya kuwa nchi inaelekea pabaya kutokana na baadhi ya watu kuamini kuwa haiwezekani kufanya siasa bila kugombana.

Askofu Malasusa alisema hata wale ambao awali walionekana kuwa ni waadilifu nao wamejiingiza katika ugomvi wa kisiasa hali inayoonesha kuwa taifa linaelekea pabaya.

Bila kumtaja mtu wala chama chochote, Askofu Malasusa alisema, “katika siasa sasa tunashuhudia watu wanaamini haiwezekani kufanya siasa bila kufanya ugomvi, hali ambayo inafanya pasiwepo amani, hali hii inadhihirisha kuwa nchi inaelekea pabaya.”

Askofu huyo pia alikemea watu wanaodhani haiwezekani kuishi bila kufanya ujanja ujanja na wale wanaoamini kuwa haiwezekani kuishi na kuongoza bila kufanya maadili mema.

Kwa upande wake, Kanisa la Anglikana Tanzania limetoa mwito kwa wananchi nchini kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya wajumbe wa Tume ya Katiba iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, juu ya mchakato wa kuandika Katiba mpya bila jazba au kutishana.

Kanisa hilo limetoa mwito na onyo hilo kupitia Askofu wa Godfrey Sehaba wa Dayosisi ya Morogoro jana mjini Morogoro wakati akitoa ujumbe wa Pasaka wakati wa ibada ya misa iliyofanyika kitaifa mkoani humo kwenye Kanisa Kuu la Utatu Mkakatifu– Anglikana, Dayosisi ya Morogoro.
Sasa taifa letu katika siku chache zijazo litaanza mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kwa lengo la kutunga Katiba mpya,” alisema Askofu Sehaba na kuongeza: Akizungumzia amani na utulivu, alisema Taifa letu kwa takribani miongo mitano (miaka 50), limejengwa katika misingi ya utu, uhuru, maendeleo, usawa, haki, kujitegemea, umoja, utaifa na uzalendo, amani na maadili, lakini yapo matukio yanayoashiria kutikiswa kwa misingi hiyo na kuleta nyufa.

Aliwataka Watanzania kuacha kulalamika juu ya hali zao za umasikini na kuwataka wafanye
kazi badala ya walio wengi kushinda kucheza 'pool' na kupiga soga huku wakilalamika hali hiyo.

Kwa upande wao, Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT), imeendelea kukemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa Serikali, Taasisi za umma na wa madhehebu ya dini ambao wanadiriki kujihusisha na ufisadi pamoja wizi wa mali ya umma, jambo linalorudisha nyuma maendeleo ya Watanzania na uchumi wa taifa.

Akitoa salamu za CCT jana katika Ibada ya Pasaka kitaifa, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Mchungaji Dk. Leonard Mtaita, alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufisadi na kufananisha na jiwe kubwa lililofunika kaburi la Bwana Yetu Kristo na kuhitajika mtu shupavu mwenye nguvu ya kuweza kuliviringisha jiwe hilo na kaburi kuwa wazi.

Alisema mbali ya hilo, jiwe jingine ni ushirikina, na wizi wa fedha na mali ya umma na kupendekeza kuwa Takukuru sasa ipambane na wezi wa fedha na mali za umma badala ya kusubiri watoa rushwa na wala rushwa pekee ili kuokoa mamilioni ya fedha zinazoibwa kila siku.

Imeandikwa na Hassan Simba, Lindi; John Nditi, Morogoro na Shadrack Sagati, Dar es Salaam
.
CHANZO