RAIS Jakaya Kikwete ameonya kuwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya usifanywe kwa kuegemea udini, ukabila, ubinafsi, siasa ama kulenga kuvunja Muungano.
“Tanzania hakuna udini wala ukabila, wajumbe wa Tume ya Katiba mnatakiwa kuongozwa na maoni ya wananchi siyo ya makundi mnayotoka, hatutaki ipatikane Katiba itakayoegemea udini, ukabila, siasa wala kulenga kuvunja Muungano, katiba ni ya Watanzania wote,” alisema Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwaapisha wajumbe wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya, Ikulu, Dar es Salaam Jana.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa maoni ya wananchi lazima yaheshimiwe hata kama hayataweza kuingizwa yote katika katiba hiyo.
Tume hiyo itaanza kazi yake ya miezi 18, Mei mosi mwaka huu, kwa kukusanya maoni ya wananchi na kutengeneza rasimu ya katiba, baadaye zikifuata hatua mbili muhimu ambazo ni kuundwa kwa Bunge Maalumu la kuchambua rasimu hiyo, kisha wananchi kupiga kura ya maoni.
Rais Kikwete ambaye alianza kuzungumza kuanzia saa 4:17 hadi 5:21 asubuhi, aliwataka wajumbe hao kuweka pembeni maslahi ya makundi wanayotoka kwa kuwa kazi wanayoifanya ni kwa maslahi ya taifa.
“Mnatakiwa kuongozwa na maoni ya wananchi sio ya makundi mnayotoka, wajumbe mliopendekezwa na vyama vyenu vya siasa mnatakiwa kutambua kuwa kazi hii sio ya chama cha siasa ni kazi ya wananchi wote,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa Tanzania haina udini wala ukabila, ingawa wananchi wake ni waumini wa dini mbalimbali, huku akisisitiza kuwa lengo ni kuwa na katiba inayoendana na wakati uliopo.
“Tanzania hakuna dini wala kabila teule, hakuna kundi wala watu wateule. Mijadala yetu kuhusu Katiba Mpya isipelekwe katika misingi ya udini wala ukabila kwani inaweza kuivuruga nchi,” alionya Rais Kikwete.
Alisema kuwa kupitia njia zote za kutoa maoni, watu wanapaswa kuzingatia sheria za nchi.
Alisema kuwa katiba mpya ni suala lililopigiwa kelele muda mrefu na watu wa kada mbalimbali, akieleza kuwa umefika wakati wale wanaosema kuwa hawawezi kushinda katika uchaguzi bila katiba kubadilishwa, kutoa maoni yao juu ya katiba wanayoitaka.
Alifafanua kwamba kuandikwa kwa katiba mpya ni historia kwa taifa kwa kuwa ni jambo ambalo halitasahaulika kwani kila mwananchi atapata fursa ya kutoa maoni yake.
“Ni historia kwa kuwa mchakato huu umepitia hatua nyingi, kwanza ilitungwa sheria, pia kutakuwa na Bunge Maalumu la Katiba na mwisho wananchi watatoa maoni yao…, lengo ni kutaka mawazo ya Watanzania ya kuiboresha katiba yao yasikike na yale yanayofaa yachukuliwe,” alisema Kikwete.
Akizungumzia uamuzi wake wa kutaka iandikwe katiba mpya, alisema kuwa kila mtu alikuwa akizungumza jambo analolijua na kufafanua kuwa ndio maana aliamua kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ili kupata maoni.
“Baada ya kukutana na makundi haya, niligundua kuwa wote tunataka kitu kimoja, sasa ni wakati wa kuipa ushirikiano tume ili ipatikane katiba itakayokidhi matakwa ya Watanzania”,
Aliongeza, “Mchakato huu ufanyike kwa amani na utulivu na kupigania maendeleo ya taifa ili kuwanufaisha watu wote.”
Wananchi wapewe nafasi
Rais Kikwete alitaka wananchi wapewe fursa bila kuwekewa vizuizi visivyokuwa vya kisheria wala kikatiba, ili waweze kutoa maoni yao kwa uhuru, huku akiwaonya wale watakaofanya njia za makusudi kuzuia watu kutoa maoni yao.
“Hata kama mwananchi atakuwa na maoni ya kijinga, aachwe atoe maoni yake, hata kama maoni yake hayawezi kuingizwa katika katiba lakini aachwe azungumze” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa kuwazuia wananchi kutoa maoni yao ni sawa na kuwanyima haki yao ya msingi, kuwataka wajumbe wa tume hiyo kuwa wavumilivu na kuheshimu mawazo ya wananchi.
Kuhusu Muungano
Alisema kuwa mchakato huo si wa kuhoji kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali ni mchakato wa kuboresha Muungano, “Lengo la mchakato huu si kuuvunja Muungano bali ni kuuboresha”.
Alisema kuwa wajumbe hao wanatakiwa kuchukua maoni yote na kuepuka vitendo vya kuyathamini maoni ya wananchi yanayofanana na sera, itikadi na mitizamo ya makundi wanayotoka.
Alisema kuwa Serikali itaipatia tume hiyo rasilimali, vitendea kazi, fedha na watu wa kuwasaidia ili waifanye kazi hiyo kwa ufanisi.
“Ulinzi na usalama wa Tume na wajumbe katika mikutano utafanywa na Serikali ili kila kitu kiende sawa,” aliahidi Kikwete.
Akitolea mfano baadhi ya mambo yanayoweza kujadiliwa na wananchi katika mchakato huo ni pamoja na namna bora ya kuendesha nchi, haki za msingi za wananchi, kuhoji namna ya kuiboresha mihimili mitatu ya Serikali, Mamlaka ya Rais, Uchaguzi Mkuu uweje na wabunge wachaguliwe vipi.
“Pia kuna suala la mawaziri kutokuwa wabunge, kuna hoja ya kuwa na wabunge wa Viti maalumu, suala la mgombea binafsi, upatikanaji wa majaji,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein alisema kuwa Zanzibar ilibadili Katiba yake kwa kupitia mchakato kama unaofanyika Tanzania Bara na kuongeza kuwa katiba hiyo ndio ilikuwa mwanzo wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Ni vyema mchakato huu tukadumisha umoja, amani na mshikamano, wananchi wajitokeze kutoa maoni yao na viongozi wa dini na siasa wachukue dhamana yao kuhakikisha zoezi hili linafanyika bila chuki,” alisema Dk Shein.
Alisema kuwa Tume hiyo ni ya Wananchi wa Tanzania hivyo inatakiwa kuungwa mkono na sio kupigwa vijembe.
Mwenyekiti wa Tume azungumza
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba aliliambia Mwananchi kuwa kazi iliyo mbele yao ni ngumu ila watajitahidi kuifanya kwa ufanisi.
“Kazi ya kukusanya maoni ni ngumu kwa kuwa tutalazimika kuzunguka nchi nzima…, baada ya kuapishwa tutakutaka kama Tume ili tupange mikakati ya kuanza kukusanya maoni,” alisema Jaji Warioba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani alisema kuwa watajipanga kuhakikisha wanakusanya maoni ya kutosha kutoka kwa wananchi.
Walioapishwa jana ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake, Jaji Mkuu mstaafu, Jaji Augustino Ramadhan.
Wajumbe wengine kutoka Bara walioapishwa ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk Sengodo Mvungi, Richard Shadrack Lyimo, John Nkolo, Alhaji Saidi El Maamry na Jesca Sydney Mkuchu.
Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Malingumu Kashonda, Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Jasmine Malale na Joseph Butiku.
Wajumbe kutoka Tanzania Visiwani ni Dk Salim Ahmed Salim, Fatma Saidi Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Saidi, Ussi Khamis Haji na Salma Maoulidi. Wengine kutoka Visiwani ni Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.
Wengine ni Katibu wa Tume hiyo, Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu wake, Casmir Sumba Kyuki.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa wajumbe hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu Pili Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wengine ni , Jaji Mkuu wa Tanzania Othman Chande, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, mawaziri, mabalozi, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa
0 Comments