ASKARI wanne wa Jeshi la Polisi nchini, wamefikishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kujipatia na kuuza dawa za kulevya zenye thamani ya Sh milioni 150.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo, askari hao walitenda kosa hilo mwezi uliopita na wamekuwa wakishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kuhamishiwa kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga.

Chanzo chetu cha habari kiliwataja askari hao kuwa ni WP Koplo Fatma, Koplo Mpelelezi Lisa, Sajini Taji Mpelelezi Atufigwegwe na Koplo Mpelelezi Mohamed ambao wote walikuwa kikosikazi maalumu cha Jeshi hilo.

Chanzo hicho kilisema baada ya askari hao kukamatwa, walifikishwa katika mahakama ya kijeshi katika Kituo Kikuu cha Polisi, lakini walimkataa msikilizaji wa kesi yao, aliyetajwa kwa jina moja la Bundala, wakidai hawana imani naye na ndipo wakahamishiwa Stakishari.
“Hivi sasa wako Stakishari na suala lao linasikilizwa na Mkuu wa Kituo hicho, Mung’ong’o, baada ya kumkataa msikilizaji wao wa awali, Ijumaa iliyopita, wakidai hatawatendea haki kwa kuwa ana maelekezo kutoka juu yakimtaka awatimue kazi,” kilisema chanzo hicho.

Kukamatwa kwa askari hao, kiliongeza chanzo hicho, kulitokana na msiri wao aliyewapa habari za kuwapo dawa za kulevya mahali fulani, kumgeuka katika makubaliano ya awali.

“Hawa askari walikubaliana na msiri aliyewapa taarifa, kwamba wakishazikamata wampe ahsante yake … badala yake walimkwepa na kuziuza dawa hizo na kuwasilisha Polisi unga ambao ulibainika kuwa ni chokaa, ili kudanganya kuwa ni dawa za kulevya kama kielelezo, kumbe walishaziuza,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa.

Baada ya msiri huyo kubaini kudhulumiwa, alitoa taraifa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, ambayo nayo iliwasiliana na kitengo cha Polisi wa Kupambana na Dawa za Kulevya na kuwakamata washukiwa hao.

Katika kufuatilia undani wa taarifa hii gazeti hili liliwatafuta baadhi ya maofisa wa ngazi ya juu wa Mkoa wa kipolisi ya Ilala na Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ambapo ilipozungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema yuko likizo na kutoa namba ya simu ya Kaimu Kamanda Saada Haji.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda Haji hakukiri wala kukataa, zaidi ya kusema tukio hilo halikutokea katika mkoa wake na majina ya askari wanaotajwa kuhusika na tukio hilo hawako chini yake, hivyo waulizwe watu wa Kanda Maalumu.



Nako Kanda Maalumu, Kamanda Suleiman Kova hakupatikana kwa maelezo ya kuwa mkutanoni, hata hivyo gazeti hili likaelekezwa kuonana na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hamisi Mhakka.

Mhakka alikiri kushikiliwa kwa askari hao wanne na kuwapo kwa kesi hiyo ya tuhuma za dawa za kulevya, ingawa alisema wakati tukio linatokea hakuwa kazini, kwani alikuwa kwenye msiba wa nduguye.

“Kweli kesi hiyo ipo na kwa taratibu watahumiwa hao wanafikishwa kwenye mahakama ya kijeshi ili kubaini ukweli wa tukio hilo ili kujua nini kilitokea na kutokana na hilo, wanashikiliwa hadi sasa kwa usalama wao, kwani biashara ya dawa za kulevya ina watu wengi nyuma yake, na wakiwa nje inaweza kuzua jambo jingine baya,” alisema Mhakka.

Chanzo chetu kilidai kuwa matukio ya uhalifu kama hayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya askari Polisi wasio waaminifu lakini wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao, tena wakifanya hivyo bila kificho.

Kilitolea mfano wa tukio la Juni 9 mwaka juzi, ambapo askari Koplo Mpelelezi (jina linahifadhiwa) akiwa na wenzake tisa, walimvamia raia aliyetambuliwa kwa jina moja la Sanga na kumpora mbolea yenye thamani ya Sh milioni 40.

“Walipokamatwa, mambo yalifunikwa, hivyo wakakubaliana kuchanga fedha zikatimia na kumlipa Sanga na mambo yakamalizika,” kilisema chanzo hicho.