Mapigano yamezuka katika eneo jengine la mpakani baina ya Sudan Kusini na Kaskazini, na huenda vita vikazidi kutapakaa.
Siku ya Jumaane, Sudan Kusini iliteka visima vya mafuta vya eneo la Heglig, ambavyo vinaleta moja kati ya pato kubwa la Sudan Kaskazini.Mapambano ya hivi karibuni, yamezusha wasiwasi kuwa vita kamili vitarudi.
Mapigano yametokea Kuek, katika jimbo la Sudan Kusini la Upper Nile, karibu na mpaka wa Sudan Kaskazini.
Kundi la wapiganaji linaloongozwa na Johnson Oliny, limeshambulia mji huo, kwa mujibu wa msemaji.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, aliiambia BBC, kwamba Kuek ilitekwa kwa muda mfupi, lakini ilikombolewa na wanajeshi wake.
Kanali Philip Aguer alilishutumu jeshi la Sudan kwamba liliwasaidia wapiganaji kwa mizinga.
Alisema Sudan Kaskazini inajaribu kuzusha vita kwengineko, kabla ya kufanya shambulio kubwa dhidi ya Heglig.
Haikuwezekana kupata taarifa kutoka jeshi la Sudan Kaskazini.
Kanali Aguer piya alisema wanajeshi wake katika eneo la Heglig limeshambuliwa kwa ndege Jumapili kutwa.
0 Comments