Na Mwinyi Sadallah.

Watu 12 wamefikishwa Mahakamani Zanzibar na kusomewa mashitaka matatu ikiwemo kupinga Muungano.
Washitakiwa hao walifikishwa katika mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe wakiwa katika Ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi Zanzibar, wakiwemo wanaharakati wanaotetea kuvunja Muungano. Walifikishwa mbele ya hakimu Omar Mcha Hamza.
Waliyofikishwa mahakamani ni Rashid Salum Ali (48) mkaazi wa Kikwajuni, Khamis Hassan Hamadi (51) wa Jang'ombe, Rashid Ali Rashid (21) Mombasa, Hashim Juma Issa (54) mkaazi wa Mbweni, Suleiman Mustafa Suleiman (31) wa Mombasa na Haji Sheha Hamadi (49) wa Chumbuni.
Wengine ni Rami Mbaraka Ahmed (48) wa Michenzani, Salum Massoud Juma (38)wa Rahaleo, Mussa Omar Kombo (67) wa Mpendae, Omar Kombo Is-hak (21) wa Magogoni, Ali Omar Omar (54) Bububu na Massoud Faki Massoud (31) mkaazi wa Kilimahewa.
Mwendesha mashitaka, Said Ahmed Mohammed alidai washitakiwa hao wanadaiwa kukusanyika barabarani wakiwa na mabango ya kupinga Muungano wa Tanganyika Zanzibar. Aidha, alidai washitakiwa hao wanadaiwa kufanya mkusanyiko usio halali, pamoja kufanya vitendo vya uhuni na uzururaji kinyume na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004 na vifungu vya 55 (1) (2) (3) na 56.
Alidai kuwa Aprili 20, 2012 saa 2:30 za asubuhi, huko Mbweni Wilaya ya Magharibi Unguja, walijikusanya katika barabara ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kusababisha hofu kwa watu wa maeneo hayo..
Alidai kuwa pamoja na Jeshi la Polisi kutoa tangazo lakuwataka washitakiwa hao kutawanyika waligoma. Washitakiwa walikana mashitaka yao, lakini uapande wa mashitaka ulisema upelelezi haujakamilika na kuomba kuiahirisha kesi na kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, watuhumiwa hao waliomba mahakama hiyo iwapatie dhamana ombi ambalo hakimu alilikubali. Kila mmoja anatakiwa kuwasilisha dhamana ya fedha taslimu Sh. 500,000 na wadhamini wawili wenye vitambulisho kikiwemo cha Mzanzibari Mkaazi, na mmoja kati ya wadhamini awe ni mtumishi wa Serikali.