Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Ahmad Masoud Ahmad, amesema wizara yake imejipanga vyema katika kuingia katika mfumo mpya wa digitali unaotarajiwa kuanza Disemba mwaka huu.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Televisheni ya ITV, Ahmad alisema wapo katika mradi wa Mkongo wa Mawasiliano unaotarajiwa kukamilika Julai mwaka huu, na karibu wilaya zote za Zanzibar wanatandika mkongo huo, ili kuwawezesha wananchi wote kuingia katika mfumo wa digitali.
Aidha, Ahmad alisema Serikali inafanya juhudi ya kuomba misaada na mikopo ili kupata meli mpya itakayomilikiwa na Serikali, ambapo amesema fedha hizo zikipatikana meli hiyo itakamilika ndani ya miezi nane hadi 10.
“Kwa sasa Serikali ina meli moja tu, Mv Maendeleo, ambayo ni chakavu. Tunafanya juhudi ili kutengeneza meli mpya na tayari tumeshaandaa taarifa kuhusu aina ya meli tunayotaka, sehemu tunayotaka itengenezwe na jumla ya abiria tunayotaka ibebe,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa chumba cha abiria Terminal 2 katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, alisema ujenzi huo umechelewa kwa sababu kuna mabadiliko yaliyofanyika katika ramani iliyokuwa imepangwa awali na kwamba nyumba ya abiria inayojengwa kwa msaada wa China itahudumia abiria milioni 1.4 kwa mwaka.
Alisema serikali imepiga hatua katika ujenzi wa barabara ambapo hadi sasa ni kilomita 350 zilizojengwa, 210 ni upande wa Zanzibar na kilomita 140 ni Pemba.
0 Comments