KILICHOIPATA Chadema Aprili 5 Arusha Mjini ndicho kimeipata CCM Sumbawanga Mjini.

Aprili 5, aliyekuwa Mbunge wa Chadema, Arusha Mjini, Godbless Lema aling’olewa ubunge baada ya Mahakama kuthibitisha kuwapo udhaifu katika uchaguzi uliomwingiza bungeni.

Baada ya siku hiyo CCM kushangilia matokeo ya kesi hiyo ya kupinga matokeo dhidi ya Lema, jana ilikuwa zamu ya Chadema nayo kushangilia, pale Mbunge wa CCM Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, alipokwaa kisiki na kung’olewa ubunge na Mahakama.

Hali hiyo ilitokana na jana Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga kutengua matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Hilaly mwaka 2010.

Mahakama ilitoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na baadhi ya hoja zilizoletwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chadema, Norbert Yamsebo aliyekuwa akitaka matokeo ya uchaguzi mkuu huo katika jimbo hilo yatenguliwe. 

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi Betwell Mmila wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, alisema: “Baada ya kupitia hoja zote, nashawishika kusema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa si wa haki na huru.”

Baada ya kusikia kauli hiyo umati uliohudhuria kusikiliza hatma ya Mbunge huyo, ulishindwa kujizuia kushangilia kwa vifijo na nderemo




Yamsebo aliitaka Mahakama hiyo ibatilishe matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo, kwa madai ya kuwapo ukiukwaji wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi na kusababisha uchaguzi huo kutofanyika katika mazingira ya haki na uhuru.

Katika uchaguzi huo, Aeshi alipita kwa ushindi mwembamba wa tofauti ya kura 196 baada ya kupata kura 17,328 wakati Yamsebo ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo, akipata kura 17,132. Rushwa Katika hukumu hiyo ambayo ilichukua saa tatu kusomwa, Jaji alielezea kuwapo kwa mazingira ya rushwa na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwa baadhi ya maeneo.

Akitaja baadhi ya maeneo hayo, Jaji Mmila alisema ni pamoja na eneo la Shule ya Msingi ya Katandala Mazoezi, ambako Aeshi alikwenda kwenye kikao cha ndani kilichodaiwa kuitishwa na viongozi wa CCM, ili kushawishi baadhi ya wapiga kura kwa kuwapa rushwa ya Sh 15,000. 
Kwa mujibu wa Jaji Mmila, watu wapatao sita walikuwa kwenye mkutano huo kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

Eneo lingine ambalo lilitajwa kuwa na dosari ni kukosekana mazingira huru katika kampeni kwenye vijiji vya Mtimbwa na Kisumba ambako mgombea wa Chadema alizuiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kufanya kampeni zake.

Mahakama hiyo mbali na kutengua ubunge huo, pia ilimtaka Aeshi alipe gharama zote za kesi hiyo. Pamoja na kutolewa kwa hukumu hiyo, Mahakama ilitoa fursa kwa upande wa mlalamikiwa kukata rufaa iwapo utakuwa haujaridhika na hukumu.

Wakili kukata rufaa Baada ya hukumu hiyo iliyovuta hisia za wakazi wengi wa mjini Sumbawanga na vitongoji vyake kutolewa, Wakili Severine Kampakata aliyekuwa akimtetea Aeshi, alisema wanakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo mara baada ya kutathmini mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Kwa upande wake, aliyekuwa mlalamikaji wa kesi hiyo, Yamsebo alisema kilio cha wanyonge kimesikika na Mahakama imetenda haki, hali ambayo inafanya wananchi kuendelea kuwa na imani na mhimili huo wa Dola.

Hii ni hukumu ya pili katika kesi za uchaguzi; kutengua matokeo jimboni baada ya hivi karibuni, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kutengua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi aliyekuwa mgombea wa Chadema, Lema.

Hata hivyo, Lema awali alidai hatakata rufaa kwa madai kwamba hataki kuwa mbunge wa mahakamani na ana uwezo wa kuibwaga CCM katika uchaguzi mdogo, lakini alibadilisha uamuzi huo na kukubali kukata rufaa baadaye baada ya kushawishiwa na chama chake. 
Naye Lucy Lyatuu, anaripoti kuwa Chadema imeelezea kufurahishwa na hukumu hiyo kwa madai kuwa ilikuwa na matumaini ya kushinda kesi ya kupinga ubunge wa Aeshi.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika alitamba jana kuwa wanachosubiri ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutangaza siku ya uchaguzi ili chama hicho kitwae jimbo hilo.

“Tutajipanga kama ilivyokuwa Arumeru … haki haikutendeka katika uchaguzi ule na tulikuwa na matumaini ndio maana kupitia Mahakama imethibitika,” alitamba Mnyika.


                                                  chanzo cha habari ni hapa.