Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini hapa, imezidiwa na idadi kubwa ya akinamama wanaokwenda kujifungua, na hata kusababisha watoto wanaozaliwa kulazwa watatu katika kitanda kimoja.

Katibu wa Hospitali hiyo, Omar Abdalla alikiri kuwepo kwa idadi kubwa ya akinamama wanaojifungua katika hospitali hiyo na hivyo kuzidiwa.

“Ni kweli hospitali imezidiwa na idadi kubwa ya akinamama wanaofika hapo kujifungua ambapo kitanda kimoja kinatumiwa kulaza watoto watatu,” alisema.

Alizitaja baadhi ya sababu zilizopelekea hospitali hiyo kuzidiwa na idadi kubwa ya akinamama wanaokwenda hapo kwa ajili ya kujifungua kwa imani kwamba watapata huduma nzuri za uhakika.

“Hospitali ya Mnazi Mmoja ni ya rufaa kwa hivyo watu wengi imani yao kubwa kwamba watapata tiba nzuri na salama,” alisema.

Akifafanua zaidi, alisema mkunga mmoja wa hospitali hiyo anawahudumia wajawazito zaidi ya 13 kwa siku wakati katika hospitali za Fuoni na Mwembeladu, mkunga mmoja hutoa huduma kwa akinamama wapatao watatu kwa siku.