Wananchi wakiangalia Nyumba ilioteketea kwa moto katika maeneo ya Kijito Upele
 Watu watatu wamenusurika kufa baada ya nyumba waliokuwa wamelala kuteketea kwa moto, huko Fuoni Kijito upele Mkoa wa Mjini Magharibi.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana ambapo moto huo uliteketeza kila kitu ndani ya nyumba hiyo, na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Akizungumza mama mwenye nyumba hiyo Khadija Mohammed, alisema akiwa amelala na wenziwe wawili, ndipo walipoushuhudia moto huo ukiteketeza nyumba na kuamshana.

“Ilikuwa usiku baina ya saa 7:30 hadi saa 8:00 tukiwa tumelala wakati natoka nje, niliona moto huo unawaka ndipo nilipowaamsha na kutoka nje, hatukuwahi kutoa kitu chochote ndani’’,alisema.
Akitihibisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi Mkoa Kusini Unguja kamishina msaidizi wa polisi, Augustine Ollomi, alisema kuwa chanzo cha moto huo hadi sasa bado hakijajulikana na jeshi lake bado linaendelea na uchunguzi ili kufahamu chanzo chake.


Kamanda Ollomi aliwataja watu hao walionusurika kufa ni Khadija Mohammed (47), Abubakar Othman (17) na mmoja alitajwa kwa jina moja Rajabu, huku mmiliki wa nyumba hiyo akiwa ni Ajuwedi Mohammed Ajuwedi (40), ambapo wakati wa tukio hakuwepo.Aidha kamanda huyo alivitaja baadhi ya vitu ambavyo vilikuwemo ndani ya nyumba hiyo kuwa ni vespa moja, Friji, baskeli, nguo za aina mbali mbali majiko ya umeme pamoja samani mbali mbali, ambapo hadi sasa hasara kamili haijajulikana.

Hata hivyo Kamanda huyo alisema kuwa hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa, mbali hasara ya vitu iliyopatikana.

(Zanzinews)