Marekani imekiri kuwa mwanaharakati wa kijamii mwenye ulemavu wa kuona, raia wa Uchina , Chen Guangcheng, anataka kuondoka nchini humo, suala ambalo limetishia kusambaratisha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili, yanayoendelea mjini Beijing.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema ni dhahiri kuwa Bwana Chen na mkewe walikuwa wamebadili msimamo wao, tangu walipoondoka kutoka ubalozi wa Marekani siku ya Jumatano.

Chen aliiambia BBC kua alitaka kushauriana na maafisa wa kidiplomasia wa Marekani, kuhusu mipango yake, lakini anaamini kuwa wanazuiliwa na maafisa wa serikali ya Uchina kumuona hospitalini, ambako anaishi kwa sasa.

Baada ya kutoroka kifungo cha nyumbani wiki iliyopita, Bwana Chen alipewa hifadhi katika ubalozi wa Marekani hadi siku ya Jumatano.

Suala hilo lingali linaangaziwa pakubwa na vyombo vya habari kuliko mazungumzo kati ya maafisa wakuu wa serikali ya Marekani na China.

Clinton azungumzia haki za kibinadam


Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Hillary Clinton, yuko mjini Beijing kwa mazungumzo yanayoangazia Korea Kaskazini na Syria.

Wakati mazungumzo hayo yalipoanza, Bi Clinton hakumtaja bwana Chen kwa jina, lakini aliangazia suala la haki za kibinadam.


Katika muda wa siku mbili zilizopita, kumekuwa na habari za kuhitilafiana, hasa kuhusu sababu zilizomfanya Chen kuondoka kutoka ubalozi wa Marekani na habari ambazo alikuwa amepewa.

Mapema hii leo Balozi wa Marekani nchini China, Gary Locke, alipinga madai kuwa Bwana Chen alishurutishwa kuondoka kutoka ubalozi wa wake.