Wagombea wa urais Abdul Moneim Aboul Fotouh na Amr Moussa
Misri imeandaa mjadala wa kwanza na wa aina yake kati ya wagombea wa urais.

Mjadala huu umewahusisha wagombea wakuu kwenye uchaguzi wa urais utakaofanyika baadaye mwezi huu. Wagombea hao ni aliyekuwa mkuu wa jumuiya ya kiarabu Amr Moussa na kiongozi wa kiislamu mwenye msimamo wa kadri, Abdul Moneim Aboul Fotouh.

Mamilioni ya raia wa Misri waliutazama mjadala huo ambao ulichukua masaa mengi kabla ya kumalizika na kupeperushwa na vituo viwili maarufu vya televisheni na vya kibinafsi.

Duru ya kwanza ya uchaguzi itafanyika tarehe 23-24 mwezi huu. Ikiwa hapatakuwa na mshindi bayana, basi duru ya pili itafuata mwezi wa sita.

Inatarajiwa kuwa huu utakuwa uchaguzi wa kwanza wa urais utakaokuwa huru na wa haki kufanyika nchini Misri.

Kura mbalimbali za maoni zinaonyesha bwana Moussa na Aboul Fotouh wakiwa mbele.

Tayari hilo limewafanya kurushiana maneno wakiwa kwenye kampeini zao.

Wakati mjadala huo ulipokuwa unaendelea bwana Amr Moussa alimkosoa mshindani wake kwa kumuhusisha na kundi shupavu la Muslim Brotherhood.


Naye bwana Aboul Fotouh, kwa upande wake, alimtaja bwana Muussa ambaye pia alikuwa waziri wa mambo ya nje kwa uliokuwa utawala wa Hosni Mubarak kama mabaki ya serikali iliyokataliwa na wananchi.

Wagombea wengine kwenye kinyang'anyiro hicho ni msomi wa kiisilamu, Muhammad al-Awwa; jaji anayesifika sana Hisham al-Bastawisi; mbunge wa chama cha kisosholisti, Abu-al-Izz al-Hariri; mwanaharakati Khalid Ali; na mwanzilishi mwenza wa chama cha Nasserist Karama Hamdin Sabbahi