Maafisa wawili wa usalama nchiniLibya wameuawa baada ya waasi wa zamani kushambulia ofisi ya Waziri Mkuu mjini Tripoli.
Mtu aliyeshudia alisema magari aina ya pick-up yenye kubeba makombora yalilizunguka jengo hilo na mapigano yakaanza.
Msemaji wa serikali baadaye alisema mapigano yamekoma.
Mashambulizi yanaarifiwa kufanywa na waasi wa zamani waliopigana kumuondoa madarakani Kanali Gaddafi mwaka uliopita ambao wanadai malipo yao walioahidiwa kupewa kwa utaratibu wa maalum.
Watu wengi waliokuwemo katika jengo hilo walikimbia akiwemo Waziri wa Fedha na Naibu Waziri Mkuu.
'Risasi kutokea ndani'
Ashur Shamis, mshauri wa habari wa Waziri Mkuu Abdurrahim al-Keib, aliiambia BBC kuwa waziri mkuu na maafisa kadhaa walikuwa salama na kwamba mapigano yaliyodumu kwa saa kadhaa yalikwisha.
Walioshuhudia walisema mashambulizi yalifanywa na wanamgambo kutoka Yafran, mji uliojaa wafuasi wa kundi la kikabila la Berber lililo umbali wa kilometa 100 (maili 60 ) kusini magharibi mwaTripoli.
Haijulikani Waziri mkuu Abdurrahim al-Keib aliko.
"Watu wengi waliolizunguka jengo hilo walilifyatulia risasi wakiwa na silaha za makombora," mfanyakazi wa serikali aliiambia AFP. "Baadhiyao waliingia katika jengo hilo na kuanza kufyatua risasi ndani," aliongeza.
Afisa mmoja wa wizara ya ndani alisema takriban askari wawili wa usalama waliuawa na wengine kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad mjini Tripoli anasema pamoja na kupatiwa fedha, waasi hao wanadai wale waliojeruhiwa wakati wa mapinduzi mwaka jana wamepewe matibabu nje ya nchi.
Mpango wa malipo ulisitishwa mwezi uliopita huku kukiwa na tuhuma za udanganyifu.
Mwandishi wetu anasema jengo hilo si mara ya kwanza kwa kushambuliwa, hili ni la pili katika kipindi cha miezi miwili, lakini mara hii kuna nguvu zaidi.
Serikali ya Libya imekuwa ikijaribu kuwashawishi mamia ya wanamgambo walioshika silaha dhidi ya Kanali Gaddafi kuzisalimisha huku kukiwa na wasiwasi kuhusu usalama.
0 Comments