SIMBA ya Dar es Salaam imefika salama Khartoum, Sudan, lakini inalalamikia inafanyiwa
visa na wenyeji wao timu ya Al Ahyl Shandy ya huko.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ilieleza kuwa wachezaji wa Simba walitelekezwa hotelini kwa zaidi ya saa tano baada ya wenyeji kuwaambia wangewafuata kwa ajili ya safari ya kwenda mji wa Shendi ambako ndiko mechi hiyo itafanyika.
Alisema wenyeji wao timu hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA), walikuwa wameahidi jana kwamba Simba wangeanza safari ya kwenda Shendi mara baada ya kupata kifungua kinywa saa tatu asubuhi, lakini hadi saa nane mchana hakukuwapo na basi lolote au mwakilishi yeyote aliyeenda kwenye Hoteli ya Safiga ilikofikia Simba, ambapo walipotafutwa walidai kwamba wamekwama kwenye foleni.
“Hali hiyo ilisababisha wachezaji na viongozi wa Simba kushinda nje ya hoteli hiyo wakiwa wamekaa nje kwenye viti vichache, huku wengine wakiwa wamesimama tu kwa muda wa zaidi ya saa mbili hadi tatu kwa vile muda wa kutoka hotelini ulikuwa umepita,” alisema Kamwaga.
Alisema kuna umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum, iliko Simba hadi mji wa Shendi na kwamba kama jana wangechelewa kuondoka wangeshindwa kufanya mazoezi jana jioni.
Kamwaga alimnukuu Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, akieleza kuchukizwa kwake na tukio hilo akisema linaonesha namna Shendi na SFA walivyojipanga kutumia mbinu za nje ya uwanja kushinda pambano hilo la marudiano.
Katika pambano la kwanza lililofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho, hivyo inahitaji sare au isifungwe zaidi ya mabao 2-0 itakuwa imefuzu hatua inayofuata.
“Sisi tulitaraji kukumbana na yote haya ambayo tunayaona sasa. Wanajua kwamba hawataweza kuishinda Simba ndani ya uwanja na hivyo wameamua kutumia mbinu chafu.
“Bahati nzuri, wachezaji wetu, benchi la ufundi na sisi viongozi tumejiandaa kikamilifu kwa mambo kama haya. Hata hivyo, tutapeleka mashitaka yetu kwa kamisaa wa mechi yetu kwa vile wao Shendi walipokuja Dar es Salaam tuliwahudumia vizuri kwa kila kitu,” alisema Rage.
Kwa mujibu wa Kamwaga kutokana na kuchelewa huko kuondoka, hoteli ya Safiga haikuwa imeandaa chakula cha mchana kwa wachezaji na ilibidi Rage na daktari wa timu, Cosmas Kapinga, waende mtaani kutafuta “vipoza njaa” kwa wachezaji.
Mchezo baina ya timu hizo unatarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii. Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano inayoandaliwa na CAF kwa ngazi ya klabu, ambapo wawakilishi wengine wa Tanzania ambao tayari wameshatolewa ni Yanga iliyotolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mafunzo iliyokuwa
ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje na Maqulmano ya Msumbiji.
Nayo Jamhuri ya Pemba ilitolewa michuano ya Kombe la Shirikisho na Hwangwe FC ya
Zimbabwe.
Mchezo wa kwanza na Shandy, Simba ilishinda mabao 3- 0, hivyo inahitaji sare ama isifungwe zaidi ya mabao 2-0 itakuwa imefuzu hatua inayofuata.
Katika hatua hiyo inayofuata kama Simba itafuzu, itacheza na moja kati ya timu nane zitakazotolewa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikivuka hapo itaingia hatua ya makundi itakayohusisha timu nane zitakazokuwa kwenye makundi mawili tofauti.
Wachezaji 19 na viongozi saba wapo kwenye msafara huo na kuwataja wachezaji hao kuwa ni
Juma Kaseja, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Derick Walulya, Amir Maftah, Juma Jabu,
Obadia Mungusa, Kelvin Yondani, Victor Costa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Patrick
Mafisango na Uhuru Selemani.
Wengine ni Haruna Moshi, Machaku Salum, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Edward Shija na
Gervas Arnold Kago. Viongozi wanaofuatana na timu hiyo ni Rage na Swedy Nkwabi.
Pia wapo Cirkovic, Kocha Msaidizi Amatre Richard, kocha wa makipa James Kisaka, daktari
Cosmas Kapinga, Meneja Nicholaus Nyagawa na Kamwaga.
Mkuu wa msafara ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hussein Mwamba.
0 Comments