Daktari Bingwa wa Maradhi ya Moyo katika Hospitali ya Edith Wolfson Nchini Israel Dr. Tamil Akiv akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanaibar Balozi Seif Ali Iddi alipotembelea Hospitali hiyo wakati wa ziara yake Nchini Israel.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakiwa katika picha ya pamoja na Watoto wa Tanzania pamoja na Wazazi wao wanaopatiwa huduma za Matibabu ya Maradhi ya Moyo kwenye Hospitali ya Edith Wolfson Mjini Telavive Nchini Israel. Kushoto ya Balozi Seif ni msimamizi wa Watoto hao Kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar Bibi Asma Othman Mwinyi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mtoto Julius Benard wa Mwanza Tanzania Bara anayesubiri huduma za Matibabu ya maradhi ya Moyo kwenye Hospitali ya Edith Wolfson Nchini Israel.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Mtoto Harith Othman Khamis wa Zanzibar na Mama yake wakati alipowatembelea watoto wa Tanzania wanaopatiwa huduma za Matibabu ya Maradhi ya Moyo Nchini Israel.
Wataalamu wa Afya wanaoshughulikia Utibabu wa Maradhi ya Moyo kutoka Hospitali ya Edith Wolfson Nchini Israel wanatarajia kuwasili Zanzibar Mwezi Septemba Mwaka huu kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuchuguza Virusi vinavyosababisha homa ya Viungo kwa watoto 1000 Unguja na Pemba.
Mkuu wa Kitengo cha Madaktari wa Moyo katika Hospitali hiyo Dr. Alia Kapusta alieleza hayo katika Kikao cha pamoja kati ya Uongozi wa Hospitali hiyo na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ukiwa Mwishoni mwa Ziara yake Nchini Israel.
Dr. Alia alisema Maradhi ya Moyo mara nyingi husababishwa na Virusi vya Homa ya Viungo ambayo mara nyingi huwapata Watoto wadogo. Alisema kwamba uchunguzi huo utakaohusisha watoto wa umri wa kati ya miaka mitano hadi kumi na tano umekuja kufuatia Zanzibar kuwa na kiwango cha juu cha watoto wenye maradhi ya moyo ikilinganishwa na Mataifa mengi Barani Afrika.
“ Utafiti huu umepangwa kufanywa mwezi wa septemba kwa vile kipindi hicho mara nyngi huonyesha kuongezeka kwa maradhi ya koo yanayopelekea kupatikana kwa maradhi ya moyo”. Alisema Dr. Alia. “ Lengo ni kutambua jee haya maradhi ya homa ya Viungo { Rheumatic Fever } hutokea kwa watoto baada ya kuzaliwa kati ya umri wa miaka mitano hadi kumi na tano “. Alisisitiza Dr.Alia.
Kiongozi huyo wa Madaktari wa moyo wa Hospitali hiyo ya Edith Wolfson alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba Uongozi wa Hospitali hiyo pia umepamnga kutoa semina kwa Madaktari wa Zanzibar ikiwa ni lengo la kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Hospitali hiyo na Zanzibar.
Alieleza kuwa hivi sasa wanaendelea na matayarisho ya Bajeti kwa ajili ya Uchunguzi wa matatizo yanayopelekea kuwepo kwa Virusi vinavyosababisha Homa ya Viungo nayopelekea maradhi ya Moyo. Zaidi ya Watoto 300 wa Zanzibar waliokuwa waksumbuliwa na maradhi ya moyo tayari wameshapatiwa huduma ya matibabu ya moyo katika Hospitali hiyo tokea Mwaka 2000.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif li Iddi ameushukuru Uongozi wa Hospitali ya Edith Wolfson kwa juhudi zake za kusaidia huduma za matibabua ya watoto kutoka sehemu mbali mali duniani ikiwemo pia Zanzibar.
Balozi Seif alisema juhudi za madaktari wa Hospitali hiyo zimepelekea kuokoa maisha ya watoto wengi ambao ndio wanaotarajiwa kuwa Viongozi wa hapo baadaye. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Blozi Seif na Ujumbe wake alipata wasaa wa kuwakaguwa watoto sita wa Zanzibar ambao wanapatia huduma ya matibabu ya Moyo.
Watoto hao ni pamoja na Abdullhafidh Masoud Mambo, Harith Othman Khamis,Hadhir Hassan Ali, Ntumwa Sheikh, Khadija Shame na Suleiman Ramadhan akiwemo pia Julius Benard kutoka Mwanza Tanzania Bara. Akihitimisha ziara yake Nchini Israel Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake alimpongeza Balozi wa Heshima wa Israel Nchini Tanzania Bwana Kasbian Nuriel Chirich kwa hatua zake alizochukuwa zilizopelekea kufanikisha vyema ziara hiyo muhimu kwa uhusiano wa Kiuchum wa pande hizo mbili.
Balozi seif alisema hayo katika Tafrija Maalum aliyoandaliwa yeye na ujumbe wake na Balozi huyo wa Heshima Nchini Tanzania hapo nyumbani kwake Mtaa wa Simtaki Irisi Mjini Televive. Alisema Balozi Kasbian amefanya kazi kubwa iliyoonyesha mwanga wa mafanikio yanayolenga kustawisha masisha yaWananchi wa sehemu hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake amemaliza ziara yake Nchini Israel na yuko njiani kuendelea na ziara yake ya Kiserikali Nchini Cuba. Balozi Seif anatarajiwa kurejea Nyumbani Zanzibar Tarehe 22 mwezi huu wa Mei Mwaka 2012.
0 Comments