Taifa Queens jana ilitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 37-33 dhidi ya Zambia katika mchezo wa mashindano ya Afrika yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Taifa Queens hadi robo ya kwanza inamalizika ilikuwa imetanguliwa na Zambia kwa bao 8-6 na kuwatia presha mashabiki na viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), waliofika kuishangilia timu hiyo.
Baada ya kufungwa juzi na Malawi kwa tofauti ya mabao machache, Taifa Queens ilihitaji
ushindi ili kurejesha matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Wachezaji wa Taifa Queens pamoja na kupata nafasi nzuri lakini wafungaji wao hawakuwa makini na kusababisha kupoteza nafasi nyingi za kufunga kwa sababu ya kukosa umakini golini.
Hata hivyo, timu hiyo ilibadilika kidogo na katika robo ya pili ilicharuka na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 20-16 na angalau kupunguza presha kwa mashabiki waliofika kuishangilia timu hiyo.
Katika robo ya tatu, wenyeji waliibuka na ushindi wa bao 28-26 kabla ya kugangamala katika robo ya nne na ya mwisho na kufanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 37-33.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mary Protas akizungumza baada ya mchezo huo alisema kuwa, ulikuwa mgumu lakini wamefurahi kulipa kisasi baada ya Zambia kuifunga Tanzania katika Michezo ya All Africa Games iliyofanyika Maputo, Msumbiji.
Alisema wachezaji wake walicheza wakiwa na mchecheto hasa baada ya kujua uzuri wa timu
hiyo na umuhimu wa kuibuka na ushindi dhidi ya Wazambia, lakini watarekebisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo.
Taifa Queens ambayo leo itakuwa na kibarua cha kucheza na Zimbabwe katika mfululizo wa mashindano hayo, ina pointi nne baada ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lesotho siku ya ufunguzi na jana kuifunga Zambia. Taifa Queens walifungwa na Malawi.
0 Comments